Muziki wetu una changamoto nyingi sana zinazoikabili. Mara nyingi tumekuwa tukiangazia yanayofanyika katika muziki wenyewe ambayo ni rahisi kuonekana, mfano aina ya muziki kwa kuigiliziana/mkumbo, au njia wanazotumia wasanii wetu katika Kufikisha kazi zao.
Lakini mimi leo nimeona niangalie upande mwingine kidogo ambao ni fursa kwa wasanii na vijana wengi ambao wanaangalia muziki kama wasanii tu, waandaji, na waongozaji video kama ndio sehemu pekee za kuweza kuingia.
Muziki ni tasnia/sekta kama sekta zingine ambazo hazijajitosheleza ili kujisimamia moja kwa moja kama wenzetu walioendelea, bado pesa zinavuja mahala ambapo kunahitaji usimamizi, bado mambo hayaendi kwa uweledi au kwa mfumo unaotambulika na kuweza kuwafanya vijana (wasanii, waandaaji, waongozaji) wawe matajiri na kuweza kusaidia makundi mengine na
kuongeza pato kwa taifa, ili tujivunie vipaji na uwepo wao.
Hapa naangalia sehemu ya uongozi ambayo inahitajika kuwaongoza wasanii wetu na kuwafanya wawe bidhaa bora ambazo zitaweza kuwasogeza kutoka hapa walipo na kupiga hatua zinazotakiwa mbele, wasanii wamekua wakiipigia kelele serikali irasimishe sanaa lakini bado wanasuasua, sasa inabidi wasanii waamke na kuamua kujinyanyua wenyewe mpaka hapo serikali itakapo amka na kuwaunga mkono, maana ni lazima watakuja tu wakiona mmesogea.
Fursa ipo kwenye umeneja, ni wakati sasa wasomi wetu ambao wana shahada mbalimbali kama masoko, uhasibu, au hata utawala wenye hamasa na sanaa wakatizamia upande huu wa muziki ambao una uhaba wa mameneja katika kuwaongoza wasanii wetu waweze kua na mipango iliyoandaliwa kitaalamu na mikakati mizuri kuanzia kujitengeneza kama bidhaa na muziki kwa
ujumla.
Inaweza kuwa labda nawaza kitu ambacho kinahitaji sijui utaalamu wa kisanaa lakini nachoona wasanii wetu wanahitaji kwa ukubwa ni watu wa kuwasimamia ili wawalipe sio mameneja ndio wawalipie vitu vyote wasanii wetu. Tunahitaji watu ambao watalipwa na wasanii, watakua chini ya wasanii.
Au ni wakati sasa wasanii wetu waanze kuangalia umuhimu wa kupata uongozi ambao utaweza kuwasimamia kila kitu kuweza kufikia malengo yao, uongozi ambao utaweza kuwatafutia matamasha ya kutumbuiza, masoko ya kuuza miziki yao, mpaka makampuni ya kuweza kuingia nayo ubia au kutangaza bidhaa zao au kua mabalozi, pamoja na kuwaongoza katika mstari ulio nyooka.
Maswali huwa najiuliza: Ni wasanii wetu wamekosa uweledi wa kuona umuhimu wa kuwa na watu watakao wasimamia kwa kuwachagua wao? Au ni kumekosekana watu mahiri wa kuweza kuonekana na wasanii ili wapewe hio kazi? Au ni watu wenyewe hawajafunguka na kuona kama kuna fursa ya kwenye muziki?
Au niseme umefika muda wa kutotafuta nani mchawi na kuanza kwa kila mmoja wao (wasanii na wenye uwezo wa kuwaongoza) kwa upande wake aone anaweza vipi kusimama na kuongeza thamani kwa mwenzake na kupeleka hili gurudumu mbele.
Ifike muda sasa wasanii waache kulalamika kuwa kuna wanaowabania, au muziki hauchezwi au serikali haisaidii kutatua matatizo yao na kuanza kuchukua hatua wenyewe kwasababu kwanza ni maisha yao na pili ni faida kwao, kwani ni wao wenyewe ndio walisababisha kusikilizwa, michango ya wengine ilikuwepo
ila ni wao walijianza ndipo wengine wakatokea.
Kuna vitu ambavyo serikali haviwezi kutusaidia mpaka tupige hatua wenyewe, cha kwanza ni hii tasnia, na ili hii tasnia ipige hatua kwa kasi inayostahili, wasanii na wadau waamue kusimama pamoja na kuanza kufanya mambo kitaalamu, kila mmoja awajibike kwa upande wake.
Wenye uwezo wa kuwaongoza wasanii wajitokeze, wasanii waamue kutafuta wenye uwezo wa kuwasimamia. Kila upande ufanye kazi kwa lengo la kuimarisha tasnia hii. Kuna vitu wasanii wetu wanakosa ambavyo vinahitaji maamuzi mazuri ili kusonga mbele.
Kwa pamoja tutafika pale tunapotakiwa kuwepo, kwa pamoja tujenge nyumba moja ambayo kila mtu anahisi anaweza kuijenga bila mchango wa mwingine.
Hii tasnia tamu, hata kwa asiyependa.
Yapasa kushika hatamu, ila mazuri kutenda.
Tena akili timamu, ni nyumba moja twajenga.
Wa karibu yumtamu, na wa mbali hato song
Makala imeandika na
Baraka Jereko