Waliokaa Kituo Kimoja Miaka Mitano TRA Wahamishwe-Waziri

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameagiza kuhamishwa kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) sehemu mbalimbali nchini ambao wameshakaa kwenye kituo kimoja kwa zaidi ya miaka mitano.

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi wa TRA wa Mkoa wa Kigoma mjini hapa jana na kuelezea alivyokasirishwa na tuhuma za rushwa zinazotajwa kuwafanya wasafirishaji wa shehena kuvusha bidhaa zao bila kulipa kodi katika forodha ya Manyovu, wilaya ya Buhigwe iliyopo katika mpaka wa Tanzania na Burundi.

Kutokana na hilo, ameagiza watumishi wote kituo hicho wahamishwe, akisema taswira mbaya inayoonekana kwa watumishi wa TRA inawafanya wafanyabiashara kutokuwa tayari kulipa kodi kwa hiari na kuipunguzia serikali uwezo wa kukusanya mapato, hivyo kukwamisha mipango ya serikali katika kuwahudumia wananchi.

Alisema anazo taarifa za vitendo vya rushwa vya watumishi hao, jeuri, ulevi na utoro kazini kwa kila mtu na jina lake na kwamba kuhamishwa huko ni hatua ya awali ya kujenga upya taswira nzuri ya TRA.

Aidha, waziri huyo ameitaka mamlaka hiyo kukusanya kodi kila penye fursa ya kuwepo kwa mapato na kwamba wasiogope kuingia gharama katika kusimamia hilo ili mradi wahakikishe malengo wanayoweka ya ukusanyaji yanafikiwa.

Awali, Meneja wa TRA Mkoa wa Kigoma, Thadeo Kaliza alisema mikakati ya ukusanyaji mapato iliyowekwa na maofisa wake imeiwezesha mamlaka hiyo kuongeza mapato kwa asilimia 17 kwa karibu miaka mitatu sasa.

Hata hivyo, alisema wigo finyu wa kodi, uchache wa watumishi na baadhi ya wilaya kutokuwa na ofisi kunakwaza jitihada za ukusanyaji kodi na kwamba mamlaka hiyo inazifanyia kazi changamoto hizo ili kuongeza maradufu ukusanyaji mapato.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Tatizo siyo kuhamisha watu
    Tatizo ni mfumo mzima wa utendaji
    Hata ukihamisha si watapena taarifa za ulaji kwa Anayekuja
    Kwanini hatujifunzi hata toka Kenya tuuuuu
    Ushauri wa bure kazi nyeti ziwe za mikataba kuanzia mwaka mmoja
    Na mtumishi apimwe na jinsi gani alivyosaidia serikali kupata Maputo
    It's easy and clear
    Nafasi zote ziwe wazi
    Hakuna wa kuteuliwa

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad