Wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa Yanga SC, wametupwa nje kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya TP Mazembe kuchapwa mabao 3-2 na Medeama ya Ghana katika mchezo wa kundi A uliofanyika kunako dimba la Essipong Sports huko Takoradi, Ghana.
Medeama walipata mabao yao kupitia kwa Enock Atta Agyei, Moses Amponsah Sarpong na Kwesi Donsu huku Mazembe wakipata mabao yao yote mawili kupitia kwa Jonathan Bolingi.
Kufuatia matokeo hayo, Medeama ambao mchezo wa mwisho watacheza na MO Bejaia watahitaji sare ya aina yoyote ili kufuzu hatua ya nusu fainali, wakati huo Yanga watakuwa ugenini wakikipiga na TP Mazembe mjini Lubumbashi, mchezo ambao utakuwa ni wa kukamilisha ratiba tu kwa upande wa Yanga.
Mpaka sasa, TP Mazembe bado wako kileleni na pointi zao 10 baada ya michezo mitano, wakishinda mara tatu, sare mara moja na kufungwa mara moja, wakifuatiwa kwa karibu na Medeama wenye alama nane, Bejaia wakishika nafasi ya tatu na pointi zao tano na Yanga wakiburuza mkia na pointi zao nne.
Hata kama Yanga itashinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya Mazembe, haitasaidia chochote katika kufuzu hatua ya nusu fainali kwasababu watafikisha pointi saba wakiwa wamemaliza mechi zote wakati Medeama tayari wamefikisha pointi nane ambazo haziwezi kufikiwa na Yanga.
Mchuano mkali umebaki kati ya Medeama na Bejaia mabapo kila timu inasaka nafasi ya kuungana na Mazembe kuelekea nusu fainali huku Mazembe pia ikihitaji kushinda ili kuongoza Kundi lao la A.