MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji na Mafuta (Ewura), imetangaza kushuka bei ya mafuta ya aina zote kwa jumla na rejareja.
Bei hizo mpya ya mafuta zimeshuka katika mikoa yote isipokuwa Mkoa wa Tanga, hasa kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa.
Taarifa ya Ewura jana ilisema bei hizo zimeshuka ikilinganishwa na toleo la bei za mafuta hayo lililopita la Agosti 3, mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, alisema katika toleo hilo, bei ya rejareja kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa imepungua kwa viwango tofauti.
Alisema kwa petroli imeshuka kwa Sh 65, dizeli Sh 63 na mafuta ya taa Sh 86.
“Bei ya jumla imepungua ambako kwa petroli ni Sh 65.31, dizeli Sh 63.39 na mafuta ya taa Sh 85.93,” alisema.
Ngamlagosi alisema kushuka kwa bei ya petroli katika soko la dunia na kupungua kwa gharama za usafarishaji/uletaji wa mafuta hayo nchini, ndizo sababu kuu zilizochangia kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la ndani nchini.
“Bei ya jumla na rejareja kwa petroli na dizeli katika Mkoa wa Tanga imeongezeka kidogo ikilinganishwa na toleo la bei za mafuta hayo lililopita la Agosti 3, 2016.
“Katika toleo hili, bei ya rejareja kwa petroli na dizeli imeongezeka kwa viwango ambavyo petroli ni Sh 50 na dizeli Sh 19. Kwa kulinganisha na matoleo haya mawili, bei ya jumla imeongezeka.
“Petroli Sh 49.61 kwa lita sawa na asilimia 2.80 na dizeli Sh 18.57 kwa lita sawa na asilimia 1.1.
“Ongezeko hili la bei limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kupokea mafuta mapya (petroli na dizeli) ndani ya Agosti 2016, ambayo yalitarajiwa kupokewa Julai 2016 na pia kutokupokea mafuta mapya kutoka katika meli ya MT. Nevaska Lady ndani ya Agosti mwaka huu,” alisema Ngamlagosi.
Hata hivyo, alisema mamlaka hiyo inawakumbusha wananchi kwamba bei kikomo ya mafuta kwa eneo husika, pia inapatikana kupitia simu zao za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kufuata maelekezo.
Alisema huduma hiyo hutolewa bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi nchini.