Kaka Yangu Julius Mtatiro, Usifuate Njia ya Waliopotea


Linaandika Gazeti la Mwananchi; ''BUNDI WA TIMUA TIMUA ATUA CUF NYAMAGANA'' katika habari kuna taarifa kuwa Viongozi waandamizi watano (5) wa CUF wilayani Nyamagana wamefukuzwa. Viongozi hao akiwemo Mwenyekiti wa Wilaya hiyo Ndg Salum Mkumbukwa, aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo Ndg Faida Potea, Mkurugenzi wa Mipango na Chaguzi Mohamed Makongoro, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Hamza Shido, Omary Abubakar Mkurugenzi wa Utawala na Nazar Nyampangula Mkurugenzi wa Siasa, taarifa hiyo ikaendelea kudai kuwa Viongozi wengine 2 wamewekwa chini ya uangalizi maalum ambao ni wakurugenzi wa Idara ya Fedha na Ulinzi.

Sababu kubwa iliyotolewa ni kuwa Viongozi hao hawakuwasilisha taarifa za mpango kazi wa ofisi yao. Ukiitazama sababu hii "KUTOWASILISHA TAARIFA ZA MPANGO KAZI WA OFISI" na kuilinganisha na adhabu ya kufukuzwa, utajiuliza maswali ambayo yanaweza kusababisha mtikisiko mkubwa wa ubongo, ni jambo haliingii akilini.

Haiitaji kuwa msomi wa chuo kikuu kujua kuwa sababu sio hiyo, ila kwa kuwa sababu yenyewe haiwezi kuwekwa hadharani, inatafutwa sababu nyingine "cover up" ya kujustify maamuzi ya kufukuzana.

Hili ni moja ya tatizo kubwa ndani ya vyama vya siasa vya upinzani, tatizo hili limeshakuwa donda ndugu ambalo limeshakuwa la kudumu kwa upinzani. Vyama hivi ambavyo vinadai na kupiga kelele ya udikteta na kuminywa kwa demokrasia nchini, ni kama vile vinatazama kibanzi kwa jicho la jirani ikiwa kwao kuna Boriti.

Kwa tafsiri ya shule na iliyo kikatiba, Chama cha Siasa** ni muungano wa watu (wanachama) wenye itikadi fulani waliopania kuishika na kuendesha serikali. Chama ni wanachama, sera na itikadi. kwa tafsiri hii vyama vingi vya upinzani Tanzania havina qualification ya kuwa vyama vya siasa, maana vyama hivyo vina wamiliki (ambao sio wanachama) ambao wakiamua iwe hivi inakuwa hivyo na wakiamua kufukuza yeyote kwa maslahi yao wanafanya hivyo. Vyama havina sera wala itikadi inayoeleweka.

Ni vigumu leo kutofautisha umiliki wa Mbowe kwa Tanzania Daima ama Protea hotel na Umiliki wake wa CHADEMA, namna anavyooperate, anavyotoa amri na kusimamia execution ya mikakati yake ni kama vile CHADEMA ni mali yake kamili ambayo anao mpango wa kuirithisha kwa wanawe.

Spika wa Bunge Tukufu la Jamhuri alijaribu kuwasihi na kuwashauri wapinzani juu ya tabia hii ya hovyo ya kufukuzana kila asubuhi. Lakini ni kama wana masikio na hawasikii na wana macho na hawaoni.

Kinachosikitisha ni pale ambapo hata Viongozi vijana ambao tulidhani wakati fulani kuwa tunaweza kushirikiana nao kuijenga TANZANIA NJEMA, nao wamekuwa wafuasi wakubwa wa hulka na mwendo huu wa upotevu. Mtatiro, kaka yangu utafukuza wangapi..? Maana watu si mawe kuwa utayageuza unavyotaka, kila asubuhi atatokea kwa kuhoji na kuuliza kwanini unigeuze, utafukuza wote..??? ili ubaki na nani..?

Imezaliwa ACT ikiwa ni alama ya kudumu ya udikteta wa MBOWE, Mtatiro unataka kuzalisha ACT nyingine..? Wakati mwingine tujifunze kupevuka kiakili, haya mambo yana mwisho. Waswahili wanasema hata mwisho una mwisho wake.....hautabaki MWENYEKITI wa MPITO milele...itendee haki nafasi yako, vijana wenzako tujivunie kuwa umeipitisha CUF katika wakati mgumu na ukaiacha salama. KUFUKUZANA hakutokuacha wewe salama wala CUF haitabaki salama.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad