TAKRIBANI shilingi bilioni 1.5 zimechangwa kufuatia matembezi ya hisani yaliyopewa jina la “Walk for Kagera” yaliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kusaidia wahanga wa Tetemeko la Ardhi lililotokea tarehe 10 septemba mwaka huu mjini Bukoba Mkoani Kagera.
Akizungumza mara baada ya matembezi hayo Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe Ally Hassan Mwinyi aliwashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza na kushiriki matembezi hayo ya hisani.
“Nawapongeza sana wadau wote mlioshiriki katika matembezi haya, mmeonyesha mshikamano mkubwa kwa umoja wenu mmeweza kuchangisha jumla ya shilingi 1,502,680,000 hii inatia faraja sana muendelee na moyo huo” Alisema Mzee Mwinyi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Kagera kuwa Serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wahanga wa tetemeko hilo wanapatiwa huduma stahiki na kwa wakati.
Balozi Kijazi aliongeza kuwa kutokana na kuguswa na tatizo hilo Serikali pamoja na Taasisi zake imetoa msaada wake ambao unakadiriwa kuwa zaidi ya shilingi bilioni moja ikiwa ni kuthamini utu wa wahanga.
“Najua kuna athari kubwa imetokea kutokana na tetemeko hili, sisi kama Serikali tunafanya kila jitihada kuhakikisha wahanga wote wanapata misaada na kurejesha huduma zote katika hali yake” Alisema Balozi Kijazi.
Awali akisoma maelezo ya tathmini ya athari za tetemeko hilo Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Abdallah Posi amesema kuwa hadi kufikia tarehe 16 idadi ya vifo ni 17, nyumba zilizoanguka zimefikia 840 huku zilizoharibika zikiwa ni 1264 na majengo 44 mali ya Taasisi za umma yameharibika.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mabalozi nchi, Balozi wa Zimbabwe ametoa pole kwa wahanga wa tukio hilo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania pale panapo hitaji msaada wao.
Matembezi hayo ya hisani kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia wahanga wa tetemeko la Ardhi yaliandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ,Ofisi ya Waziri Mkuu na Ikulu.