Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli amepokea taarifa ya maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi lililotokea katika Mkoa wa Kagera kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Tetemeko hilo limetokea Kagera na mikoa jirani ya Mwanza, Geita na Kigoma.
Pamoja na kupokea taarifa hiyo Rais Magufuli amepokea mchango wa fedha taslimu kiasi cha Dola za Kimarekani laki mbili (USD-200,000/-) sawa na shs 437 milioni kutoka kwa Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni.
Pia amepokea taarifa ya mchango wa mabati, blanketi na magodoro vyenye thamani ya Shilingi za Kitanzania milioni 115 kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mh Uhuru Kenyatta kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera.
Katika taarifa yake Majaliwa amesema tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu 17, majeruhi 440, nyumba 2063 zimeanguka, nyumba 14,081 zipo katika hali hatarishi na nyumba 9,471 zimepata uharibifu mdogo, huku watu 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.