Ester Bulaya Kuwekwa Kikaangoni Jumatatu

ESTER Bulaya, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, mkoani Mara anatarajia kupanda kizimbani Jumatatu ya tarehe 17 Oktoba, mwaka huu ili kutoa ushahidi wake katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge inayomkabili, anaandika Charles William.

Bulaya atalazimika kuhojiwa na kujibu maswali ya mawakili wa upande wa walalamikaji kwa upana zaidi baada ya kiapo chake kuingizwa katika kumbukumbu za Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza.
Hatua hiyo inakuja baada ya Jaji Noel Chacha wa mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi lililowekwa na Costantine Mutalemwa, wakili wa waleta maombi ambaye alikuwa akiomba baadhi ya aya zilizopo katika hati ya kiapo cha Bulaya zifutwe.

Tundu Antiphas Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ndiye wakili wa Bulaya katika kesi hiyo ambapo amepiga kambi mkoani Mara kwa takribani wiki mbili sasa wakati shauri hilo likiendelea.

Katika kesi hiyo namba moja ya mwaka 2015, walalamikaji ni watu wanne wakiongozwa na Magambo Masato, watu hao wamejitambulisha kama wapiga kura katika jimbo la Bunda Mjini huku Steven Wassira, aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa ni miongoni mwa mashahidi wa upande wa walalamikaji.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad