Ilikuwa kama mchezo wa kuigiza kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro baada ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Emmanuel Mkumbo kufikishwa ili apandishwe kizimbani kujibu mashtaka sita, likiwamo la kutishia kuua.
Tukio zima la kumpeleka mahakamani, kumpandisha kizimbani na kumsomea mashtaka kwa muda wa dakika 30 hivi lilitawaliwa na vituko. Kwanza, ni jaribio la kuwaficha wanahabari.
Kabla ya kufikishwa mahakamani, Polisi mkoani Morogoro iliwaarifu wanahabari kuwa ingetoa taarifa kuhusu mkurugenzi huyo lakini saa 4:30 asubuhi wakati Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Ulrich Matei akijiandaa kuzungumza nao, alipigiwa simu akatoka nje ya ukumbi na aliporejea alisema hawezi kutoa taarifa tena na akaondoka.
Waandishi walipofika mahakamani saa 5:00 asubuhi walikuta Kamanda Matei akishuka kwenye gari na alipanda tena akasogea kando kuzungumza na baadhi ya askari wake.
Pili, baada ya hakimu kumaliza kusikiliza kesi hiyo, Mkumbo hakurudishwa mahabusu mahakamani hapo kama ilivyo ada ili kusubiri utaratibu mwingine badala yake mshtakiwa huyo alihamishiwa chumba cha hakimu ambacho hakikuwa na kesi inayoendelea.
Humo ndugu zake walimpelekea koti kubwa jeusi na kofia aina ya pama, hivyo alitoka akiwa tofauti na alivyoingia akiwa na fulana yenye rangi nyeupe, bluu na nyeusi. Baada ya kuvaa alitoka akiwa amezingirwa na polisi, huku ndugu wakiwazuia wanahabari kumpiga picha.
Mashtaka dhidi yake
Mkumbo ambaye ni mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam alipandishwa kizimbani kujibu mashtaka sita, la kwanza likiwa la kutishia kuua kwa bastola na la pili ni la usalama barabarani lenye makosa matano.
Alisomewa mashtaka hayo na mawakili wa Serikali Sunday Hyera na Edgar Bantulaki. Katika shtaka la kwanza, mbele ya hakimu Agripina Kimaze anadaiwa Oktoba 15, saa 10:30 jioni alitenda kosa la kutishia kuua eneo la Mkambarani, Manispaa ya Morogoro.
Anadaiwa katika shtaka hilo la jinai namba 226 la mwaka 2016, alitishia kumuua kwa bastola askari namba 5057, Koplo Tuti Ndaga wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro, kinyume na kifungu namba 89 (1),(2),(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu namba 16.
Katika shtaka la pili la ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani lenye makosa matano, ilidaiwa kuwa; kwanza, siku na muda huo eneo la Mbuyuni Mkambalani, mshtakiwa alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Prado lenye rangi ya kijivu bila kuwa na leseni.
Pili, ilidaiwa alikuwa akiendesha gari hilo ambalo halikuwa na bima; tatu, alikutwa akiendesha kwa mwendo kasi; na nne, alikataa kupeleka gari Kituo cha Polisi cha Kingoluwira kama alivyoamriwa na askari, WP namba 5392 Sajenti Anna.
Ilidaiwa katika shtaka la tano kwamba, wakati akiendesha alisimamisha gari katikati ya barabara kuu ya Morogoro-Dar es Salaam kwa uzembe, bila uangalifu wala kuzingatia watumiaji wengine wa barabara. Mkurugenzi huyo alikana mashtaka yote yanayomkabili.
Hakimu Kimaze alitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa kwamba awe na mdhamini mmoja kwa kila shtaka, yaani shtaka la jinai na la usalama barabarani lenye makosa matano, wote wawe wakazi wa Morogoro na mmoja akitakiwa kuweka dhamana ya Sh500,000 kwa kosa la kwanza na Sh1 milioni kwa kosa la pili.
Mshtakiwa alikidhi masharti ya dhamana na kuachiwa huru, huku gari likiendelea kushikiliwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Morogoro.
Hakimu Kimaze aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 31, usikilizwaji wa awali utakapoanza baada ya upande wa mashtaka kudai upelelezi umekamilika.
Kadha pigwa chini chezea Magufuli kibarua kishaota Majani...walizoea utawala wa Shemeji ukiwa bosi basi una nyanyasa kila mtu na bado.
ReplyDeleteJamaa kashatumbukiwa long time sasa tutafanana kitaaa....
ReplyDelete