Baada ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kusema kuna dawa za kutosha nchini, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema ukosefu wa dawa unaojitokeza hivi sasa ni wa muda mfupi.
Waziri Ummy amekanusha taarifa zilizokuwa zimeenea kwamba kuna uhaba wa dawa za binadamu na kusisitiza kuwa, zipo nyingi na zinaendelea kuingia nchini. Pia, Waziri huyo alithibitisha kuwapo vifaatiba vya kutosha na kwamba, chanjo za watoto ndizo zilikuwa zimeisha lakini hivi sasa tayari zimeletwa.
Hata hivyo, kauli hiyo inakinzana na ya Samia aliyoitoa wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa wodi ya wazazi Hospitali ya Mwananyamala.
Samia alisema ukosefu wa dawa unaojitokeza hivi sasa ni wa muda mfupi, kwani Serikali inajipanga kuondoa tatizo vifaatiba.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo baada ya kuelezwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Daniel Nkungu kuwa wamekuwa wakikabiliwa na upungufu wa dawa.
Samia amesema licha ya Serikali kujipanga kukabiliana na tatizo hilo, uongozi wa hospitali hiyo unatakiwa kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato.