Shahidi Aeleza Askofu Gwajima Alivyofikishiwa Bastola

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa washtakiwa watatu walipeleka bastola kwa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima wakati amelazwa katika Hospitali ya TMJ baada kubaini wanaihifadhi kinyume cha sheria.

Ofisa Upelelezi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sajini Abogasti (46) alidai hayo jana wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kushindwa kuhifadhi silaha inayomkabili Gwajima na wenzake Yekonia Bihagaze, George Mzava na Geoffrey Milulu.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shedrack Kimaro kutoa ushahidi wake, Sajini Abogasti alidai kuwa Bihagaze, Mzava na Milulu, walipeleka silaha kwa Gwajima wakati akiwa amelazwa katika Hospitali ya TMJ.

Alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha kuwa Mkuu wa Upelelezi Kinondoni alimuunganisha na Mkuu wa Kituo Kawe, Pamphil ambaye alimkabidhi begi lililokuwa na bastola namba CAT 5802, risasi tatu zilizokuwa katika kasha lake (magazine), CD mbili, risasi 17 za bastola na kitabu cha umiliki silaha, chupi na hati ya kusafiria ya mchungaji huyo.

Wakili Kimaro alimtaka shahidi huyo kuionesha Mahakama kitabu cha umiliki wa silaha, shahidi alihangaika kutafuta kwa zaidi ya dakika mbili bila mafanikio na baadaye akadai ameshakirejesha kwa Gwajima.

Akiendelea kutoa ushahidi, Abogasti alidai baada ya kukabidhiwa begi hilo katika Kituo cha Polisi Osterbay alianza kufanya upelelezi lakini Gwajima alikuwa Arusha kwenye mkutano wa Maaskofu pamoja na washtakiwa wenzake.

Alidai Machi 26,2015 Gwajima alipewa wito wa kufika Kituo cha Polisi Dar es Salaam, kesho yake alifika na aliwaachia washtakiwa wenzake begi lililokuwa na silaha, na washtakiwa hao walikaa nalo kwa siku mbili jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.

Shahidi huyo, alidai kuwa Gwajima aliitwa Polisi kwa kosa la kumdhihaki Askofu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polcarp Kardinal Pengo lakini wakati akihojiwa, alipata maradhi ya ghafla na kupelekwa Hospitali ya Temeke, kisha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuhamishiwa Hospitali ya TMJ kutokana na hali yake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad