Upepo Mkali Waezua Nyumba 44 Musoma

Upepo mkali ukiambatana na mvua umeezua nyumba 44 katika Kijiji cha Kiemba Kata ya Ifulifu, Wilaya ya Musoma mkoani Mara.

Kati ya nyumba hizo, tano ziliathirika vibaya kiasi cha kusababisha wamiliki wake kulala nje. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikagua baadhi ya nyumba zilizoathirika ili kuona athari za uharibifu huo.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Vicent Naano na viongozi wa halmashauri, walitembelea eneo hilo baada ya kupata taarifa za athari za kuezuliwa paa na kuagiza tathmini ifanyike ili Serikali iweze kutoa msaada kwa wananchi hao.

Profesa Muhongo aliwaambia waathirika hao kuwa Serikali ya Rais John Magufuli ipo pamoja nao na ametumwa kuwapa pole kutoka kwa viongozi wa juu wa Serikali.

“Ndugu wananchi, nimetumwa na Rais wetu Dk John Magufuli niwape pole sana kwa kukutwa na kadhia hii ya kuezuliwa na upepo kwa paa za nyumba zenu. Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanawapa pole pia na wanawatakia heri wale wote walioathirika,” alisema.

Profesa Muhongo aliwaelekeza viongozi wa kijiji hicho wahakikishe wanafanya tathmini ya kweli kwa kupita kila nyumba iliyoathirika na yoyote atakayegundulika amedanganya ili Serikali imlipe, zoezi zima litaahirishwa na kurudiwa upya, pia wahusika watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Aliwaahidi wananchi hao kuanza kupewa misaada baada ya kikao cha halmashauri kupitia taarifa ya tathmini kesho, na kuwaelekeza viongozi kufanya kazi hiyo kwa haraka.

Profesa Muhongo alikuwa mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya kukagua umeme na kushiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere iliyofanyika nyumbani kwake Butiama juzi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad