Wasira Atumia Saa 2 Kupinga Ushindi wa Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya Mahakama Kuu Mwanza

Shahidi wa tatu katika kesi namba moja ya mwaka 2015 ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo la Bunda Mjini, Stephen Wasira leo amepanda katika kizimba cha mahakama kuu kanda ya Mwanza, inayoketi mjini Musoma kutoa utetezi wake, huku ulinzi mkali wa askari polisi wenye silaha za moto, mabomu ya machozi na mbwa ukiwa umeimarishwa.

Wasira ambaye alitumia muda wa saa 2 na dakika 26 kutoa ushahidi wake huku akihojiwa na wakili wa mlalamikiwa wa kwanza Ester Bulaya, ameiambia mahakama kuu chini ya jaji Noel Chocha kwamba uchaguzi katika jimbo la Bunda mjini ulikuwa haramu kutokana na kugubikwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni kulikofanywa na msimamizi wa uchaguzi kufuatia kuwepo kwa ongezeko la vituo vya kupigia kura kutoka 190 hadi 199, sambamba na ongezeko la idadi ya wapiga kura kutoka watu 69,369 hadi 164, 794 bila taarifa yoyote.

Mwanasiasa huyo mkongwe, ambaye aliangushwa na mgombea wa chama cha demokrasia na maendeleo ( CHADEMA ), katika uchaguzi mkuu uliopita kwa kura 19,000 dhidi ya 28,568 alizopata mshindi Ester Bulaya, amemlalamikia msimamizi wa uchaguzi jimbo la Bunda mjini kuongeza vituo 9 kwenye kata za kabasa, Bunda mjini, Bunda stoo, Manyamanyama, Nyamakokoto, Wariku na Guta pamoja na kuhamisha kituo cha Mchalo na kukipeleka mahali kusikojulikana bila kuvishirikisha vyama vitano vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo.

Mapema wakili Tundu Lissu, baada ya kupitia kiapo cha shahidi huyo Stephen Wasira aliiomba mahakama hiyo kuondoa aya ya 3b, kirumi i (ii), ( iii ) na ( iv ) pamoja na 3c, ambazo zingewezakuleta mambo mapya katika shauri hilo kinyume na masharti ya 23 ya kanuni za uendeshaji wa uchaguzi za mwaka 2013 kama zilivyofanyiwa marekebisho, hoja ambayo ilikubaliwa na jaji Noel Chocha.

Mara kwa mara jaji chocha alilazimika kuingilia kati kwa kumtaka wasira kujibu maswali ya wakili Tundu Lissu, huku Wasira akionekana dhahiri kuwa na majibu ya kujiamini; ambayo wakati mwingine yaliwafanya wasikilizaji kuangua kicheko hasa pale alipodai kuwa hamfahamu katibu mkuu wa Chadema Dk. Vincent Mashinji zaidi ya Dk. Wilbroad Slaa, ili kujiridhisha iwapo Ester Bulaya aliwahi kujaza fomu ya bajeti za gharama za uchaguzi ambayo kisheria hupelekwa kwa msajili wa vyama vya siasa mwenye uwezo wa kumwekea pingamizi mgombea aliyekiuka utaratibu.

Kipindi cha mchana kilianza kwa mawakili Costantine Mutalemwa, Yasin Memba na Hajra Mungula wanaowatetea wapiga kura wanne wa jimbo la Bunda mjini waliofungua kesi hiyo mahakama kuu kanda ya Mwanza kumhoji shahidi huyo wa tatu Stephen Wasira baada ya wakili Tundu Lissu kuhitimisha maswali yake.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad