ACT-Wazalendo walaani kauli ya Serikali kutowajengea wananchi......Wadai kauli hiyo ni fedheha kwa waathirika na Wadau.

Watanzania wanakumbuka kuwa mnamo tarehe 10 Septemba, 2016 lilitokea tetemeko la ardhi katika eneo la Kanda ya Ziwa na hususan Mkoa wa Kagera.

Tetemeko hilo lilisababisha athari mbalimbali zikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa makazi na miundombinu ya umma na watu binafsi. Jumla ya Watu 117,721 wameathirika kwa kupoteza makazi yao, mali na athari za kisaikolojia katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba, Karagwe na Kyerwa.

Aidha, jumla ya watu 17 walipoteza maisha na 560 walijeruhiwa. Vilevile, nyumba 2,072 za makazi zilianguka kabisa na nyumba 14,595 za makazi zilibomoka, baadhi zina kuta au kupata nyufa kubwa na hivyo kuzifanya kuwa hatarishi kwa makazi ya binadamu. Vilevile, maafa haya yalisababisha uharibifu mbalimbali wa miundombinu ya barabara na majengo ya watu na taasisi mbalimbali, ikiwemo shule na Hospitali.

Kufuatia maafa hayo, wananchi na taasisi mbalimbali, pamoja na nchi marafiki, waliitikia wito wa kuwasaidia wahanga wa maafa na kukarabati miundo mbinu iliyoharibika. Hadi kufikia mwezi Oktoba, Fedha, Vyakula na Vifaa mbalimbali vya Ujenzi vilikuwa vimepatikana kwa njia ya michango mbalimbali.

Chama chetu kimeshtushwa na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwamba Wananchi walioathirika wajitegemee wenyewe na kwamba misaada yote iliyotolewa Ni ya Serikali na Taasisi zake tu. Kauli hii ya Mkuu wa Mkoa haikubaliki kwani inadhalilisha waathirika na watu wote waliojitoa kuwasaidia waathirika hao.

Tunachukulia kauli hii kama tangazo la wizi wa uaminifu wa wananchi waliochanga. Ni busara ya kawaida kuwa hatua ya kwanza katika kushughulikia maafa ni kurudisha hali ya maisha ya watu katika hali ya kawaida sambamba na ukarabati wa miundombinu. Aidha, suala la ujenzi wa miundo mbinu ya taasisi za umma ni jukumu la msingi la serikali. Kwa sababu hii:

• ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuu kujitenga na kufuta kauli ya mkuu wa mkoa wa Kagera kwa sababu inaigombanisha serikali na wananchi inaowaongoza.

• ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuelekeza ni misaada iliyopatikana kwa michango ya wananchi, taasisi na nchi rafiki katika kusaidia wananchi walioathirika kurudi katika maisha ya kawaida, ikiwemo ukarabati na ujenzi wa nyumba za kuishi.

• ACT Wazalendo tunatoa wito kwa taasisi za kiraia nchini kuchukua nafasi yake katika kuendelea kuikumbusha serikali wajibu wake wa msingi wa kuboresha maisha ya watu.

Janeth Rithe
Katibu wa Taifa ACT Wazalendo, Kamati ya Maendeleo ya Jamii
13/11/2016, Dar Es salaam.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad