Hatma ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), ilishindwa kujulikana jana baada ya mawakili wa Serikali kuweka pingamizi, wakipinga Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha kusikiliza maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na mawakili wa mshtakiwa.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Jaji Sekela Moshi, alisema kutokana na pingamizi hiyo, atasikiliza hoja za sheria zilizowasilishwa mahakamani hapo kabla hajatoa uamuzi wowote juu ya dhamana ya mshtakiwa.
Aliwaelekeza mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha hoja za sheria kabla mahakama haijaendelea na hatua yoyote.
Jaji Moshi alisema atatoa uamuzi kuhusu mvutano huo wa sheria, Novemba 22, mwaka huu
Katika maombi hayo namba sita ya mwaka 2016, Jamhuri iliwakilishwa na mawakili, Matenus Marandu na Paul Kadushi wakati Lema anatetewa na jopo la mawakili sita ambao ni Peter Kibatala, John Mallya, Adam Jabir, Sheck Mfinanga, Faraji Mangula na Charles Adiel.
Katika shauri hilo jana, hoja za sheria za pingamizi zilianza kusikilizwa saa 4:54 asubuhi hadi saa 7:25 mchana ambako mawakili wa Serikali na wale wa upande wa utetezi, walichuana vikali kujenga hoja.
Akiwasilisha pingamizi hilo, wakili Kadushi, aliiomba mahakama iwaruhusu kuwasilisha pingamizi moja na kama mahakama ikishindwa kuridhia pingamizi hilo, wawasilishe pingamizi la pili.
Alidai maombi hayo yaliyosainiwa na wakili Kibatala yanalenga katika kifungu cha 372 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinachoipa Mahakama Kuu kufanya mapitio ya mashauri ya kesi za mahakama za chini.
Alidai hoja ya sheria inasema mabadiliko ya sheria yaliyofanyika mwaka 2002 yaliondosha haki za pande zote katika kesi za jinai kuomba rufaa au mapitio ya uamuzi mdogo uliofanywa katika mahakama zinazoongozwa na mahakimu nchini.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 43 (2) cha sheria ya mahakama za mahakimu, maombi hayo yanakinzana na kifungu hicho kwani uamuzi huo mdogo unaopingwa na mawakili wa mshtakiwa, haujamaliza shauri la jinai.
“Lakini pia, uamuzi huo unaobishaniwa na mawakili wa mshtakiwa, uko katika ukurasa wa 17 hadi 19, hivyo mahakama inafungwa na sheria kusikiliza rufaa au mapitio katika uamuzi mdogo.
“Kwa kuwa uamuzi ni mdogo mahakama inakuwa na uamuzi wa kutupilia mbali maombi haya na kusubiri tuendelee na mwenendo wa kesi. Lakini, kama mahakama haitavutiwa au kushawishiwa na hoja hii, tunaomba kutoa hoja ya pili,”alidai wakili Kadushi
Baada ya hatua hiyo, hoja ya pili iliwasilishwa ikisema maombi ya Lema hayajakidhi matakwa ya sheria, kifungu cha 359 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2,002.
Kwa mujibu wa wakili Kadushi, kifungu hicho kinaelekeza namna mtu asiporidhika na uamuzi uliotolewa na mahakama ya chini, anavyotakiwa kukata rufaa mahakama kuu.
“Msingi wa sheria umeshawekwa na mahakama kuwa maombi ya kufanya mapitio kamwe siyo mbadala wa rufaa na uamuzi mwingi umetamka hivyo,” alidai wakili Kadushi.
Katika maelezo yake, wakili huyo alirejea mashauri mbalimbali ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa yenye kesi za namna hiyo na kudai kuwa kulikuwa na haki ya waleta maombi kukata rufaa na haki hiyo ipo mpaka sasa.
Wakili Kibatala
Kibatala ambaye alikuwa akiwawakilisha mawakili wenzake watano, alidai hoja za sheria zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri hazina msingi katika sheria na akaiomba mahakama izitupilie mbali.
Aliiambia mahakama kwamba hakimu aliyeruhusu wakili wa Serikali kusimama kabla hajafikia mwisho wa uamuzi aliokuwa akiusoma ni ishara kuwa mahakama hiyo haikuongozwa vizuri jambo ambalo linaifanya Mahakama Kuu iingilie kati na kutoa maelekezo.
“Hoja walizoleta Serikali hazijakidhi matakwa ya sheria. Kwanza kabisa, pingamizi lao halijasema linakuja kwetu au linakwenda kwa mahakama kwa sababu sisi na Serikali tumeitwa hapa mahakamani na hii ni kama mwananchi wa kawaida kwenda kwa msajili kulalamika kisha jaji akaziiita pande zote mahakamani,” alisema Kibatala.
Alisema wanaishangaa Serikali kuzungumzia kifungu cha 43 ambacho barua ya maombi yao haijakizungumza na pia mahakama kuitisha majalada na kupitia yaliyotokea mahakama za chini, inajenga mamlaka na kuruhusu mahakama kuu kuitisha majalada hayo kupitia mwenendo au uamuzi.
“Kifungu cha 373 cha sheria hiyo ya makosa ya jinai, kinaelezea jinsi Mahakama Kuu inavyoweza kupata taarifa ya upungufu wa mwenendo katika mashauri yanayoendelea mahakama za chini.
“Mfano mahakama za chini zinaruhusiwa zenyewe kupeleka majalada mahakama kuu ili kupitia mwenendo au kupata taarifa yoyote au kuomba namna ya kurekebisha wanapokosea na hata mwanasheria mkuu wa Serikali amewahi kutumia mfumo huu katika kesi mbalimbali,” alisema Kibatala.
Alisema mahakama kuu ina mamlaka ya kupokea malalamiko na kuyafanyia kazi na ina uhuru wa kuitisha majalada na kusikiliza maombi ya upande wowote kati ya Serikali au utetezi.
Katika maelezo yake, Kibatala alisema kifungu cha 148 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinasema rufaa inaweza kukatwa kama mtu amenyimwa dhamana ila uamuzi wa mtu kunyimwa dhamana haukatazi mshitakiwa kuomba mapitio ya uamuzi huo.
“Mahakama ilijivua mamlaka ambayo inayo ikiwa ni pamoja na kazi yake ya sheria. Katika hili, hakimu alikosea kumruhusu wakili wa Serikali kusimama katikati ya uamuzi.
“Nasema hivyo kwa sababu kifungu cha 148 (6) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinasema mahakama ikitoa dhamana kwa mshitakiwa ni lazima ifikie mwisho wa hatua ya uamuzi wake kwa kuweka masharti ya dhamana.
“Lakini katika suala hili, mahakama iliishia njiani baada ya wakili wa Serikali kuingilia kati na kueleza kusudio la kukata rufaa.
“Jukumu letu ni kuiongoza mahakama na siyo kuviziana ili tushinde. Hapa Kadushi amedai haturuhusiwi kuomba mapitio au rufaa ila akasema tulipaswa kukata rufaa na siyo kuomba mapitio ya mwenendo wa uamuzi ule.
“Kwa misingi hiyo, ndiyo maana tunasisitiza kwamba pingamizi la Jamhuri halina mashiko yoyote ya sheria, tunaomba litupiliwe mbali na mahakama isikilize maombi yetu,” alisema Wakili Kibatala.
Katika maombi hayo, Lema kupitia mawakili wake, anaiomba mahakama hiyo ifanye mapitio ya majalada ya kesi za jinai namba 440 na 441 ya mwaka huu ambako anakabiliwa na makosa ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli
Mawakili hao wa Lema wanaomba ombi hilo kwa sababu wakati Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Desderi Kamugisha akisoma mwenendo wa uamuzi huo uliokuwa na kurasa 22 hivi karibuni, alisema mahakama hiyo inamwachia Lema kwa dhamana kwa masharti atakayopewa na mahakama hiyo.
Hata hivyo, kabla hajakamilisha uamuzi huo akiwa katika ukurasa wa 21 kati ya kurasa 22, mawakili wa Serikali walisema Serikali inakusudia kukata rufaa juu ya uamuzi huo.
Wakati hayo yakiendelea, jana nje ya mahakama kuu, kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi na askari magereza waliokuwa na silaha za moto.
Mungu atakusaidia. Amen
ReplyDelete