Pia ni kampuni inayojihusisha na machapisho ya kazi za wasanii iliyowasaini, kuratibu uzalishaji na utengenezaji, usambazaji, kutafuta na kukuza masoko na utekelezaji wa haki miliki za nyimbo na video za muziki za wasanii iliyowasaini, kufanya ‘scouting’ katika mashindano mbalimbali ya kukuza vipaji na kuendeleza vipaji hivyo.
Tasnia yetu ya Bongo flava imekua na mlipuko mkubwa sana na sasa imeshakuwa ni kama fashion kila msanii au mtu ambaye hajawahi hata kuwepo kwenye industry kuibuka na kudai kuanzisha record label ya kusimamia baadhi ya wasanii ambao hata haifahamiki wamewapata wapi na nani aliyegundua kua wana kipaji na ni wasanii ambao ni promising.
Awali producer mkongwe nchini P-Funk Majani aliwahi kuwa na record label ambayo ilifahamika kama Bongo Records iliyosimamia kazi za wasanii mbalimbali kuanzia studio, kushoot video, kusambaza kwenye media na wakati mwingine hata kuandaa tour za mikoani kwa ajili ya shows.
Wasanii kama Jay Mo, marehemu Mangwair, Juma Nature, Daz Nundaz walikuwa ni kati ya members wa label hiyo. Ilichukua miaka kadhaa kwa tasnia ya Bongo Flava kupata record label nyingine kama ilivyokuwa kwa Bongo Records hadi mwaka jana ambapo msanii Diamond Platnumz alitangaza kuanzisha record label yake ya WCB, ambayo nayo inafanya vizuri sana ndani na nje ya nchi ikisimamia kazi za wasanii wake ambao ni Rich Mavoko, Ray Vanny na Harmonize kuanzia rekodi za audio, video, kusambaza kwenye TV na kwenye vituo mbalimbali vya redio.
Jambo la kuchekesha ambalo kwangu naliona kama ni halina mantiki ni kwamba tangu WCB ianze kuwa record label na kusimamia kazi za wasanii mbalimbali na kuonesha mafanikio kiasi, pameibuka mlipuko wa wasanii wengi wa Bongo Flava na hata wasio wasanii kudai nao wameanzisha record labels na wanasimamia wasanii na jambo hili nimeliita ‘Kupatwa kwa record labels’
Nilibahatika kutazama interview ya Diamond akifanyiwa mahojiano na mtangazaji Lil Ommy wa Times FM na alikiri wazi kuwa investment aliyoifanya kwa kuwasimamia Harmonize, Mavoko na Ray Vanny bado haijaanza kumlipa na anatarajia labda baada ya miaka miwili ndio huenda ikaanza kumlipa.
Just imagine kwa wasanii wanaofanya vizuri kama hao na kufanya show nchi mbalimbali za jirani lakini bado kiasi kilichowekezwa hakijaanza kurudisha faida hali. Vipi kwa Gaucho wa Shilole ambae sijawahi kusikia akifanya hata show za mikoani?
Record Label ni kampuni na ili kampuni yoyote ifanikiwe lazima iwe na mipango na maono ya mbali. Lazima iwe na uwekezaji wa kutosha, lazima pawe na mikakati na usimamizi unaoeleweka, lazima uajiri watu wa masoko, watu wa mahesabu na pia lazima uwe na mkwanja mrefu na connections za kutosha.
Unawezaje kuanzisha record label ya kusimamia wasanii wengine ilhali wewe mwenyewe bajeti yako ya video ni milioni 2? Unawezaje kusimamia wasanii wengine ilhali wewe mwenyewe huwezi kujisimamia? Hujawahi hata kufanya show yako peke yako zaidi ya kuwa msindikizaji show za wasanii wengine na matamasha kama Fiesta halafu leo useme unasimamia msanii mwingine?
Kuwa na kiasi kidogo cha pesa cha kuweza kulipia msanii kurekodi na kufanya video haimaanishi unaweza wa kusimamia msanii au kuanzisha record label. Kumiliki studio yako chumbani sio kigezo cha kumsimamia msanii. Una impact gani katika muziki? Una connections za kutosha? Una exposure gani katika muziki nyumbani na kimataifa?
Wasanii hebu fikirini mara mbili.
Imeandikwa na Javan Watson