Mwanafunzi Apigwa Risasi na Polisi Dar, Askari Wawili Watiwa Mbaroni


Mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari Gerezani, Shakil Sures amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya kujeruhiwa kwa risasi na polisi kwenye mazingira ya kutatanisha. 


Tukio hilo lililotokea Jumatatu eneo la Fire, Upanga licha ya watu kusikia milio ya risasi, kushuhudia polisi wakipita na kumuona kijana huyo akiwa tayari kajeruhiwa, lakini hakuna mwenye maelezo sahihi kuhusu nini kilitokea hadi askari hao wakachukua hatua hiyo. 


Baadhi ya waliokuwapo eneo la tukio siku hiyo walidai kuwaona askari waliokuwa eneo hilo wakirusha risasi, bila kujua walikuwa wakipambana na nani. 

Mmoja wa mashuhuda, Athumani Simba alidai walidhani ni majibizano ya risasi kati ya askari na majambazi, baada ya kuona gari la polisi likipita eneo hilo. 


“Niliwaona askari wawili wakielekea eneo la Fire huku wakipiga risasi, ghafla nilimuona mwanafunzi akilia huku akiwa ameshika mguu wake akiomba msaada,”alisema Simba. 

Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema mwanafunzi huyo alifikishwa hospitalini hapo jioni ya Jumatatu na kwamba jeraha lake linaendelea vizuri. 


“Tumempokea mwanafunzi Shakil juzi jioni na kidonda chake kimesafishwa na kinaendelea vizuri,” alisema Aligaesha. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Hamduni Salum alisema upelelezi kuhusu tukio hilo unaendelea. Hata hivyo, hakueleza mazingira ya tukio lenyewe yalivyokuwa. 


“Tunawashikilia askari polisi wawili waliokuwa zamu siku hiyo ya tukio, upelelezi unaendelea ili kuangalia kwa nini walitumia nguvu kubwa kiasi hicho,”alisema Kamanda Salum.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. KUNATISHA
    WANAOHUSIKA NA UJAMBAZI WENGINE WANAOPIGWA RISASI WENGINE.
    USALAMA UKO WAPI?

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad