Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba amesema Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA linapaswa kubadili mfumo wa ufanyaji kazi kwakuwa kwa sasa linafanya kazi kama polisi kuliko kuuendeleza muziki wa Tanzania.
Akiongea kwenye kipindi cha XXL Ijumaa hii, Ruge alisema baraza hilo limekuwa likionekana zaidi katika kuwaadhibu au kuwafungia wasanii kuliko kusaidia kukua kwa muziki ikiwemo kutoa milango zaidi kwa watu wanaotaka kuanzisha tuzo.
“Mlolongo wa tuzo unakuwa ni mgumu wakati ni jambo ambalo linatakiwa kupewa msukumo mkubwa sana. Baraza la sanaa, na vyombo vingine vimekuwa vikifanya zaidi ya upolisi kuliko kusukuma,” alisema.
Amedai kuwa kutokana na BASATA kupenda kufungia video au nyimbo, wasanii wamekuwa wakifanya makusudi kwakuwa kazi zao hupata kiki na video zao Youtube kupata views zaidi zinazowapa fedha kuliko kazi kuchezwa kwenye TV.
Anaamini kuwa baraza hilo linapaswa kuwa mbele kiteknolojia na kimawazo kuliko hata wasanii wenyewe na kuweza kwenda na mabadiliko ya muziki duniani.
Ruge amedai kuwa hata muziki wa dansi umeporomoka kwasababu hakuna chombo cha muziki ambacho kinawasaidia.