Inasemwa kuwa “wewe ni kile unachokula” kwa kumaainisha kuwa mwonekano wetu na afya ya mwili na akili unajengwa na chakula tunachokula. Madhara ya chakula chetu tunachotumia yako pia katika ngozi. Kuna vyakula vinavyozeesha ngozi kwa haraka na ni budi kuvijua na kuviepuka.
Vyakula hivi japo tunavipenda sana lakini vina athari mbaya kwa miili yetu na muhimu kujenga tabia ya kuviacha katika milo yetu. Kama si rahisi kuacha kabisa basi angalau kupunguza matumizi yake.
Vifuatavyo ni vyakula 7 vinavyozeesha ngozi na unashauriwa kuvitoa katika mlo wako:
1. Nyama Nyekundu
Mojawapo ya vyakula vinavyozeesha ngozi ni nyama hasa nyama nyekundu. Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa nyama nyekundu inayotokana na wanyama kama ng’ombe,mbuzi,kondoo,nguruwe n.k ni mbaya kwa afya njema ya binadamu na hivyo kwa ngozi pia. Nyama nyekundu ina kemikali aina ya carnitine ambayo inafanya mishipa ya damu kukakamaa na kusababisha kuzeeka kwa ngozi.
Hivyo nyama nyekundu ni mojawapo ya vyakula vibaya kwa afya ya binadamu na vya kuvizuia.
2. Chumvi
Chumvi hasa yenye madini ya iodine ni mbaya sana kwa afya ya ngozi. Inasababisha chembechembe za nyama katika ngozi kuvimba.
[Soma zaidi kuhusu chumvi: Madhara ya Kula Chumvi Nyingi kwa Afya ya Binadamu]
3. Sukari
Sukari japo tunaipenda sana ni adui mkubwa wa afya ya binadamu. Inadhoofisha mfumo wa kinga za mwili. Kiasi kingi cha sukari mwilini kinafanya ngozi kuwa kavu na kufanya mwili utengeneze makunyazi kwa sababu inaharibu kemikali ya collagen na elastin ambazo zinafanya kazi ya matengenezo ya ngozi kuifanya isiharibike na kuwa chakavu.
Sukari nyingi inasababisha mwili kukosa nguvu ya kupambana na bacteria wabaya. Ongezeko la bacteria hawa kunafanya utengenezwaji wa kemikali mbaya ambazo husababisha uchakavu wa ngozi.
Watu wanashauriwa kutumia sukari asilia kama ya matunda na asali kuliko zile zinazopatikana katika vinywaji kama soda na pipi , jojo,biskuti au vitafunwa vingine vyenye sukari ya kuongeza.
4. Vyakula Vya Kukaangwa
Vyakula vya kukaangwa kama chipsi,nyama za kukaanga vinasababisha uingizaji wa mafuta mengi mwilini. Mafuta haya yenye vitu vinavyoitwa “Free Radicals” yanasababisha uzibaji wa vijitundu katika ngozi. Ukiachia ngozi mafuta mengi mwilini yanasababisha madhara mengi mengine yakiwemo magonjwa ya moyo na kisukari.
5. Mkate Mweupe,Tambi Na Keki
Vyakula hivi vina kemikali ya glucemic kwa kiwango kikubwa ambayo inaleta madhara ya magonjwa ya ngozi (Ugonjwa wa madoa katika ngozi)
6. Pombe
Unywaji wa pombe unasababhisha kupoteza maji mengi mwilini kwa njia ya mkojo na huleta madhara mabaya kwa ngozi kwa kuifanya iwe kavu.
7. Kahawa (Caffeine)
Kemikali ya caffeine iliyomo katika kahawa na vinywaji vingine inasababisha ukosefu wa maji ya kutosha katika ngozi na kuifanya iwe kavu. Lakini pia caffeine inasababisha utengenezwaji wa kemikali ya cortisol ambayo inachangia uzeekaji wa ngozi.
Badilisha Tabia Yako Ya Ulaji
Vyakula hivi ni baadhi ya vingi ambayo vimo katika ulaji wetu wa kila siku na una madhara makubwa kwenye ngozi zetu. Wanawake wanaathirika sana na ngozi ukilinganisha na wanaume. Au niseme wanajali sana ngozi zao kuwa zenye afya na kuvutia kuliko wanaume hivyo wanaweza kufaidika sana kwa kupunguza au kutotumia kabisa hivi vyakula vinavyozeesha ngozi.
Fahamu kuwa afya yako ni mtaji mkubwa hivyo ni kitu muhimu kuipa afya ya mwili wako kipaumbele na hivyo zingatia ulaji wako.