WATU wanaopenda kujibadilisha miili na ngozi zao kwa kutumia vipodozi vyenye kemikali za kujichubua na kubadilisha mwonekano wa sehemu za maumbile yao wametajwa kuwa miongoni mwa watu wanaosumbuliwa na matatizo ya kisaikolojia.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Penina Mlama alisema wanawake na wanaume ambao wanatumia vipodozi hivyo wana matatizo ya kujiamini, hivyo huchukua uamuzi wa kujibadilisha.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa kimataifa kati ya Shirika la Codersia na Majumuhi (Pan African) ya Kigoda cha Mwalimu Nyerere wa kujadili mabadiliko ya mwili ambayo yamekuwa yakifanywa na watu mbalimbali.
Alisema watu wamekuwa wakifanya mabadiliko kwa kujichubua, kujichora mwilini (tattoos), kuongeza maumbile bila kujua kuwa kuna madhara makubwa ya kufanya hivyo.
“Mabadiliko haya yana madhara makubwa kiafya na kijamii…wengi wanaojibadilisha hawajiamini na wana matatizo ya kisaikolojia, mabadiliko haya yana gharama kubwa sana, lakini hata baada ya kupata madhara pia ni gharama,” alisema Profesa Mlama na kuongeza kuwa, katika mkutano huo wataangalia kiini cha kujibadilisha, huku akiainisha kuwa baadhi ya watu wanaojibadilisha wanafanya hivyo kutokana na msukumo katika jamii na kutaka wafanane na watu wengine.
Msomi huyo alisema kwa hapa nchini, tatizo kubwa la kujichubua lipo kwa wanaume na wanawake na baada ya mkutano huo wataangalia zaidi eneo lingine lililoathirika zaidi.
“Tutafanya utafiti kwa nini watu wanaongezeka kwenye madhara ambayo ni gharama, kwa nini wanafanya hivyo na kama wana elimu ya kutosha juu ya wanachokifanya,” alisema.
Naye Katibu Mtendaji wa Codesria, Ebrima Sall alisema, pamoja na kwamba watu wanaofanya hivyo wana matatizo ya kisaikolojia, lakini pia wataangalia namna ya kuzishauri serikali namna ya kudhibiti matumizi ya vipodozi hivyo.
Alisema watajaribu kuangalia namna ya kushauri watunga sera, serikali na vyombo vinavyohusika na biashara namna ya kuzuia vipodozi hivyo, kwa kuwa vimekuwa vikihusika katika kutoa vibali vya kuingizwa kwake.
Sall alisema suala la watu kujibadilisha miili yao limekuwa tatizo kubwa duniani, huku akieleza kuwa kwa Afrika hilo linakuwa ni jambo la kushangaza kwa sababu wanawake na wanaume wamekuwa wakiacha utamaduni wa Kiafrika.