AUAWA Kwa Kuchomwa Kisu Wakati Wakigombea Soda

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia mkazi wa Olasiti, jijini Arusha, Hamisi Amani (17), kwa tuhuma za kumuua mwenzake wakati wakigombea soda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, tukio hilo lilitokea Desemba 25, mwaka huu, saa mbili usiku katika eneo la Kwa Morombo.

Kamanda Mkumbo alimtaja marehemu kuwa ni Novatus Tadei (26), mkazi wa Kwa Morombo na kwamba aliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani upande wa kushoto.

“Marehemu na mtuhumiwa walikuwa wapishi kwenye kampuni inayojulikana kwa jina la ZZ Catering inayomilikiwa na Bashiri Ally.

“Siku ya tukio, marehemu pamoja na wafanyakazi wengine, akiwamo mtuhumiwa, baada ya kumaliza kazi waliyokuwa wanafanya, walipanda gari lenye namba za usajili T 375 CHH, aina ya Toyota Hiace wakirejea nyumbani.

“Wakiwa ndani ya gari hilo, mtuhumiwa Hamis aligundua kuwa soda aliyokuwa ameiweka ndani ya begi lake, haipo na kuanza kuhisi marehemu ndiye aliyeichukua.

“Kwa hiyo, ulizuka ugomvi baina yao na kuanza kutukanana matusi. Wakati ugomvi huo ukiendelea, mtuhumiwa alimkaba marehemu na kuchukua kisu wanachotumia kwenye shughuli zao za mapishi kilichokuwa ndani ya vyombo na kumchoma kifuani.

“Baada ya kuchomwa kisu, Tadei alianguka chini na jitihada za wafanyakazi wenzake waliokuwamo ndani ya gari hilo kuokoa maisha yake zilishindikana, kwani alifariki wakati anapelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu,” alisema Kamanda Mkumbo.

Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamilika.
Tags

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. du kweli bongo maisha ni magumu kweli mtu anamuua mtu yaani sababu ya soda tu? mimi nakunywa soda mpaka namwaga nikishindwa kumaliza, ndiyo maana sielewi yaani mtu anawezaje kumuua mtu sababu ya soda, kama siku moja nilisoma katika mtandao kuna jamaa alimuua kaka yake sababu ya pombe ya kienyeji ya shilingi mia mbili hayo mambo yanatokea huko kwenu bongo tu maana hapa Ulaya sijawahi kusikia mtu kaua mtu sababu ya soda, chakula wala pombe

    ReplyDelete
  2. du jamaa anaweza kufungwa jela kifungo cha maisha sababu ya soda

    ReplyDelete
  3. Hapana hamko sawa kwa mnayoyasema, ukifuatilia utakuta visa vya namna hii vinaanzia mbali sana na hivyo mioyo inajengeka na sumu ya uhasama! Ndiyo sababu unatakiwa pale unapokuwa umefanyiwa jambo baya na ukawa na maamuzi ya kusamehe, basi usamehe kwelikweli tena 70X70 lkn ukiweka moyoni ipo siku utatenda na kuhitimisha ZAMBI kubwa!

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad