NSATO Marijani, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Jeshi la Polisi pamoja na vigogo wengine wa serikalini wanatuhumiwa kushindwa kumsaidia Mtanzania Abdulswamadu Zacharia Omary (36) anayedai kutendewa vitendo vya kikatili, anaandika Josephat Isango.
Ukatili huo ni pamoja na kudhulumiwa mali na wafanyabiashara Said Sadi na Ghalib Said Mohamed.
Akisimulia mkasa huo huku akilia, kijana huyo anadai kufanyiwa vitendo vya kikatili ikiwemo kutaka kunyongwa ndani ya chumba cha mahabusu kilichopo Kituo cha Polisi Oystebay, kitendo anachosema kiliratibiwa na jeshi hilo kuwasaidia wafanyabiashara hao kupoteza ushahidi lakini amekuwa akilalamika bila kusaidiwa.
“Nimekuwa nikitumiwa na baadhi ya vigogo wa polisi wanajidai kutaka kunisaidia lakini wakifika kwa huyu jamaa wanakaa kimya, polisi wanashirikiana na huyu aliyekuwa mmiliki wa Home Shoping Centre (HSC), kutesa watu, na mimi wanakataa kunilipa milioni zaidi ya 250, nilizofanyia kazi nikiwa kwao Yemen,” anasema Omary.
Akisimulia mkasa wa tukio, Omary anasema alipewa zabuni ya kujenga jengo la ghorofa 3 nchini Yemen bila kupewa mkataba, akakataa lakini alinyang’anywa hati zake za kusafiria na kuteswa kikatili hali iliyopelekea akubali.
“Nilisaidiwa na watu wa shirika la kimataifa la wahamaji (International Organisation for Migration) kurudi Tanzania, lakini tangu nimerejea nchini, hawa jamaa wa iliyokuwa Home Shoping Centre na GSM wana nguvu serikalini hadi ndani ya vituo vya polisi,” anasimulia.
Katika barua yake ambayo amewaandikia viongozi kadhaa wa taasisi za serikali ambayo MwanaHALISI online imeiona Omary amesema, viongozi hao wamewekwa kwenye mfuko na wafanyabiashara hao, kiasi cha kuifanya serikali idharaulike.
“Unasikia, hili suala linajulikana pote polisi, afande Marijani analipotezea kwa muda mrefu, nilielekezwa kwa afande wa Interpol anaitwa Ngonyani.
“Pia Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, (Takukuru) wanalifahamu lakini ndugu yangu kila aliyetaka kunisaidia huishia kukaa kimya, natamani sasa kumwona rais anisaidie,” anasisitiza.
Omary katika andishi lake ametaja hata viongozi wa dini ambao wamekuwa wakijipatia fedha kutokana na tatizo lake ambalo polisi wameshindwa kulifanyia kazi.
Ninatishwa, ninaambiwa hawawezi kufanywa lolote ndani ya nchi hii, wakisikia nimelalamika kwenye ofisi yeyote ya serikali hata polisi hunijibu “wewe unapolalamika unaenda kwao, sisi tunawaita wanakuja tulipo, unajihangaisha.”
Anadai tarehe 23 Julai 2015 alitekwa na Gharib Said Mohamed pamoja na Faisal kisha kupelekwa Masaki na kwamba, alipigwa na akawa hajitambua.
“Nilipojitambua nilijikuta Kituo cha Oysterbay nimefunguliwa mashtaka likiwemo la kumtukana rais, kutaka kulipua Ikulu, kukutwa na silala na niliwekwa rumande siku 46 bila kufikishwa mahakamani na namba ya jalada ilikuwa OB/IR/6365/2015, na OB/IR/11770/2015.
Nilipofikishwa mahakamani nilikuta mashtaka tofauti ambayo yalifutiliwa mbali na hakimu sababu hayakuwa ya kweli.
MwanaHALISI Online, limewasiliana na afande Lucy Ngonyani, aliyeshughulikia suala hilo na kukiri kuwa, analifahamu, yupo likizo na yeye sio msemaji wa jeshi hilo.
Alipoulizwa Nsato Marijani, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo alisema, “huyo kijana anapaswa afike ofisini kuniona, kama suala lake halijatekelezwa sio kuja huko kwa vyombo vya habari.”
Mtandao huu uliwatafuta watuhumiwa hao (Said Sadi na Gharib Sadi Mohamedi) kupitia simu zao za mkononi, pamoja na simu zao kuita kwa muda mrefu, hazikupokelewa.
Na hata walipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu zao, hawakujibu.
Chanzo:Mwanahalisionline
Ni Hatari kwa Taifa kama linawalinda Wahujumu wa nje na kuwafunika Wazalendo nchini. Hii ni kati ya migogoro mingi CCM ipo haitaweza kujitoa hapo. Kwenye ubia na vigogo, ambao walikataa kuimalizia Katiba ili nchi ifuate sheria wakiogopa kubanwa na sheria za nchi. Kule kubebana kwa wakuu ndio janga na tatizo la mfumo wa CCM. Mpaka CCM itolewe madarakani na Katiba ya Wananchi irudi ndipo Tanzania itafunguka. Angalia Ghana iliingiliwa na wawekezaji wengi lakini ukiangalia maendeleo na uzalendo umekufa. Sababu inaendeshwa na wageni si Waghana wenyewe. Pesa kitu kichafu, kinatupeleka nyuma enzi za mkoloni ingawa tumekaa madarasani huko tuliimba tu. Moyoni hatuko hivi. Kama unaiuza nchi, na uko radhi kumnyanyasa Mtanzania kwa pesa, Tanzania imekwisha. Kama jeshi letu pia linatumika basi nchi iko wazi inachezewa kama bao. Na usalama wa nchi upo hatiani. Tatizo Wajinga wengi tumejaa Tanzania. Tunaongea lugha za kigeni maarifa hatuna. Dado tupo wajinga. Tatizo ni mmoja, huwezi kunfundisha mjinga sababu uelevu wa kujiona yeye ni mjinga hana.
ReplyDeleteHapa CCM, inahusika na nini? acheni polojo, uenda anayefanya haya ni kada wa upinzani na anaipaka matope ccm, nenda mbali and think out side the box. Uhalifu hauna itikadi na ndiyo maana uanaitwa uhalifu.Kama suala hili lina ushaidi wakutosha basi taasisi husika wafuatilie na kubaini ukweli wa jambo hili. Viongozi tuache kasumba za kusubiri kila kitu ofisini mwisho wa siku ni kashfa na fedhea kwa serikali na nchi kwa ujumla wake. Taarifa hii ni chanzo cha taasisi husika kuanza kufuatilia kwa kina na kulifanya suala hili kuisha maramoja. Hpa sioni inapohusika ccm, labda kwa kuwa kila mtu kwa nchi amekuwa mwana siasa badala ya kuwa mjasilia mali na ndiyo maana kila mtu analia hakuna hela. Heela zipo tena nyingi ila sisi atutaki kubadilika na kuacha wachache kwenye siasa na wengi kuwa na shughuli nyingine za kutuongezea kipato.ALUTA CONTINUA.....
ReplyDelete