Wadau wa soka nchini wameendelea kumlilia mchezaji Ismail Halfan wa timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 wa Mbao FC ya Mwanza, aliyefariki dunia Desemba 4, 2016 baada ya kuanguka kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera
Mchezaji Ismail Mrisho Halfan wa timu ya Mbao U-20 akitolewa uwanjani na watu wa msalaba Mwekundu baada ya kuanguka uwanjani wakati wa mchezo wao uliokuwa .
Akizungumzia msiba huo, baba mzazi wa Ismail, Halfan Mrisho akiwa Jijini Mwanza ameelezea kupokea kwa masikitiko msiba huo, na kusema kuwa hiyo ni kazi ya Mungu, na kwamba mambo ya michezo ndivyo yalivyo.
Halfan amesema pia msiba huo ni pigo kubwa kwa taifa kwa kuwa mwanaye alikuwa na ndoto kubwa katika soka la Tanzania na alikuwa mahiri katika nafasi yake.
Kwa upande wake moja ya wanafamilia ambaye pia ni mlezi katika kituo ambacho Ismail alikuwa akilelewa, bwana Felicious, amesema kituo hicho kimepata pigo kubwa kumpoteza Ismail katika mazingira hayo kwani alikuwa ni moja ya wachezaji ambao walikuwa na ndoto kubwa.
"Ismail alikuwa tayari amepata nafasi ya kwenda kwenye kituo kimoja cha soka nchini Marekani, alikwenda kwa wiki mbili kufanya majaribio, akafaulu, na alirudi nchini kumalizia mitihani yake ya kidato cha nne, ili aende rasmi kwenye kituo hicho, lakini imekuwa bahati mbaya, kazi ya Mungu haina makosa" Amesema Felicious.
Mwili wa marehemu unataraji kuwasili Mwanza leo kwa ajili ya taratibu za maziko.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetuma salamu za rambirambi na kusema kuwa limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha kushtukiza cha Mchezaji huyo wa timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 wa Mbao FC.
Timu hiyo ya Vijana wa Mbao, kama vilivyo timu nyingine 7 za Ligi kuu ya Vodacom, ilikuwa Kituo cha Bukoba katika Ligi ya vijana ambayo kwa msimu huu imefanyika kwa mara ya kwanza.
Timu nyingine Nane zilikuwa kituo cha Dar es Salaam.