KILICHOJIRI Katika Mgomo wa Saa 24 Wachezaji wa Yanga

WACHEZAJI wa Yanga jana walifikisha siku ya pili sawa na saa 24 tangu wakubaliane kuweka mgomo wa kutofanya mazoezi ya timu hiyo uliosababishwa na madai ya mshahara wao wa Novemba, mwaka huu.

Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo, George Lwandamina kwa mara ya kwanza juzi Jumatatu asubuhi alishuhudia mgomo huo wa wachezaji tangu aanze kibarua cha kukinoa kikosi hicho.

Yanga wameweka mgomo huo, ikiwa ni siku chache tangu waanze vyema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa mabao 3-0 walioupata dhidi ya JKT Ruvu.


Ishu nzima ilikuwa hivi, Jumatatu wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo walifika mazoezini yaliyotakiwa kuanza saa mbili na nusu Uwanja wa Uhuru, Dar.

Mara baada ya wachezaji na benchi hilo kufika uwanjani, kama inavyokuwa kawaida mipira na vifaa mbalimbali vinavyohusiana na mazoezi viliwekwa uwanjani tayari kwa kuanza programu mbalimbali za mazoezi.

Wakati, Lwandamina na benchi lake la ufundi wakiendelea na maandalizi ya kuanza programu za mazoezi, ghafla kocha huyo alishangaa kuona wachezaji wakiwa hawana hata mpango wa kufanya mazoezi hayo kutokana kila mmoja kutojihusisha na chochote.

Championi Jumatano, liliwashuhudia wachezaji hao baadhi wakiwa wamekaa kwenye mti aina ya mwarobaini ulikuwepo pembezoni mwa uwanja wakipiga stori zao huku wakiwa wamevalia mavazi yao ya kawaida.

Wakiwa uwanjani hapo, majira saa ya 3:15 asubuhi Lwandamina pamoja na Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi wa timu hiyo Mholanzi, Hans van Pluijm walionekana wakizungumza na wachezaji hao, lakini baadaye saa 4:00 asubuhi viongozi waliingia kwenye basi na kuondoka zao uwanjani hapo.

Basi hilo, liliondoka uwanjani hapo likiwa na viongozi wote pamoja na kiungo Mzambia, Justine Zulu huku wengine wakibaki uwanjani hapo wakiwa na magari yao.

Dakika chache baadaye tangu viongozi hao waondoke, wachezaji waliitana kwa wale waliokuwa kwenye magari kushuka na kukaa kikao kujadiliana kuhusiana na suala hilo na kufikia muafaka wa kutofanya mazoezi hadi pale watakapolipwa mshahara wao.

Kikao hicho, kilitumia dakika tano pekee kilichoanza saa 4:10 hadi 4:15 na baada ya hapo wakaagana na kuondoka zao uwanjani kwa wale wenye magari kuwapa lifti wenzao.

Jana Jumanne, wachezaji hao waliendelea na mgomo huo kwa kutotokea kabisa uwanjani baada ya Lwandamina na Pluijm pamoja na benchi la ufundi kufika uwanjani hapo na basi la timu na kujikuta wakiwa wapo peke yao.

Basi hilo, lilifika kwenye Uwanja wa Uhuru saa 2:15 asubuhi kwa ajili ya mazoezi, lakini walipofika wakakuta uwanja mweupe huku kukiwa hakuna mchezaji yeyote, hivyo wakalazimika kusubiri kwa dakika kadhaa kisha basi hilo likageuza na kuondoka katika eneo hilo.

Kwenye basi hilo, hakuwepo mchezaji yeyote zaidi ya viongozi hao wa benchi na watunza vifaa vya timu ambao walipofika uwanjani hapo hakuna yeyote aliyeshuka kwenye basi na badala yake kukaa ndani.

Mara baada ya kuondoka uwanjani hapo, Championi Jumatano, halikuishia hapo lilifuatilia basi kujua wapi wanaelekea na ndiyo ghafla basi hilo likaingia kwenye sehemu ya maegesho ya kituo cha mafuta Chang’ombe.

Dakika chache baadaye, likafika gari aina ya Toyota Harrier lililoegeshwa mbele ya basi hilo huku waandishi wa gazeti hili wakiwa wamejificha.

Ghafla akashuka Pluijm akaenda kuingia kwenye gari hilo akakaa kwa dakika tatu na baadaye akashuka akaelekea kwenye basi na kuingia Lwandamina.

Lwandamina akiwa amevalia nguo za mazoezi, naye akaingia kwenye gari hilo na kukaa kwa dakika tano kisha akashuka kurudi katika basi na kisha akamalizia meneja, Hafidh Saleh aliyekaa kwa dakika chache kabla ya basi hilo kuondoka katika eneo hilo.

Basi hilo, liliondoka katika eneo hilo saa 5:02, asubuhi na kuelekea kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Jangwani na basi hilo lilipofika hapo viongozi hao wakashuka na kuingia ofisini humo.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa timu hiyo, Baraka Deusdedit kuzungumzia juu ya hilo alisema “Hilo suala lipo kwa uongozi na linashughulikia malipo hayo ya mshahara na wakati wowote kuanzia hivi sasa watalipwa.

“Hivyo, tarajia kuwaona wachezaji wetu wakiendelea na mazoezi kama siyo leo (jana) au kesho (leo) baada ya malipo yao kukamilika,”alisema.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Tatizo nini?pesa hakuna au boss Manji katia ngumu kulipa?Kama ndio hivyo wakina mzee Akilimali wako wapi,si wachukue jukumu la kulipa mshahara wachezaji kama Manji kawachunia,au kelele tu kwa waandishi wa habari.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad