Mimi Mchange Habibu Mchange, Leo Jumaamosi tarehe 10.12.2016, ninaujuza umma wa Watanzania, Rafiki zangu, ndugu na jamaa. Kwamba kwa kipindi kirefu sasa nimekuwa nikijihusisha na harakati za kisiasa, awali nikiwa mwanachama wa Chadema na baadae ACT WAZALENDO.
Kwamba katika Chama cha ACT WAZALENDO nimepata heshima ya kuwa kiongozi mwandamizi kama katibu wa Mipango na Mikakati na baadae Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa katika secretarieti ya Chama hicho.
Na Kwamba tangu kujiunga kwangu na Chama hicho nimekuwa mjumbe wa kamati kuu, mjumbe wa Halimashauri kuu na Mjumbe wa Mkutano mkuu wa Chama.
Kwa moyo mkunjufu kabisa, na kwa mapenzi mema na taifa langu.
Ninathibitisha Kwamba nimejitoa rasmi katika ushiriki wa aina yote ya siasa ili nipate muda mwingi zaidi kufanya na kusimamia shughuli zangu za kijasiriamali zinazonitaka nitoe fursa na huduma Sawa kwa viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa.
Kwa mantiki hiyo basi, kuanzia Leo hii, nitaiomba jamii katika yote nitakayofanya inione nimefanya kama Mchange huru asiye mwanachama wa Chama chochote cha siasa.
Ninaomba uamuzi wangu huu uheshimiwe na kamwe nisihusishwe na aina yoyote ya siasa bali utanzania wangu.
Ningeweza kufanya uamuzi wangu huu kimya kimya, lakini kwa hatua niliyoifikia na ili kuweka kumbukumbu sawia ni budi niutoe kwa umma.
Ninafahamu kuwa kuwa mwanachama wa Chama cha siasa ni haki yangu ya kikatiba, lakini nimeamua kuihifadhi haki yangu hiyo kwa sasa Mpaka hapo nitakapoona inafaa kufanywa vinginevyo.
Ninawatakia kila la heri waliokuwa wanachama wenzangu wa ACT WAZALENDO katika kuyafikia malengo ya msingi ya uanzishwaji wa Chama hicho.
Kujiondoa kwangu kushiriki katika siasa kusihesabiwe kama sehemu ya kukwamisha au kurudisha nyuma matarajio na au malengo ya Chama hicho.
Tafadhali ichukueni hii kama chachu ya kuwafanya mfikie malengo mahsusi kwa wakati muafaka bila kurudi nyuma.
Msivunjike moyo, msirumbane, pendaneni,heshimianeni na shikamaneni ili mfikie lengo
Sasa nitabaki na kuendelea kuwa ndugu yenu, rafiki na swahiba. zaidi mtanzania mwenzenu. Tutaendelea kushirikiana katika mambo yote ya kijamii na kimaisha yasiyohusiana na mlengo wa kiitikadi wa kisiasa.
Kwa wanachama wa vyama vinginevyo kama CHADEMA, CUF, CCM, ADA TADEA na kadharika, nitaendelea kuwa rafiki mwema kwenu, jirani na ndugu wa kweli kama au pengine zaidi ya ilivyokuwa hapo awali.
Ninawatakia heri wanasiasa wote wa vyama vyote hapa nchini.
Ninawaomba radhi wote niliowahi kuwakosea, kuwa kwaza ama kuwafanya wajisikie vibaya kutokana na matendo yangu, maandishi yangu Misimamo yangu, matamshi yangu ama na mwenendo wangu wa kisiasa kwa kipindi chote nilichokuwa mwanachama wa vyama vya siasa hapa nchini.
Ninaahidi kuendelea kuwa mtanzania Mtiifu mwenye mapenzi mema kwa taifa langu huku nikiwatakia heri wanachama wapenzi na viongozi wa vyama vyote vya siasa.
Itoshe tu kufahamika Kwamba Mimi *Habibu Mchange,* kwa sasa si mwanachama, mpenzi wala mshabiki wa Chama chochote cha siasa.
Zaidi, Ninawaomba radhi watu wote ambao kwa namna moja ama nyingine nitakuwa nimewakwaza kutokana na uamuzi wangu huu.
Natanguliza shukrani zangu za dhati.
Wasalaam
Habibu Mchange,
0762178678.
Morogoro Tanzania