KIWANGO cha Pesa Kesi za Mafisadi Kushushwa Chini ili Kuwabana Wengi

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema serikali inatarajia kujadili kushusha kiwango cha fedha kinachohusika katika makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kwenye mahakama ya mafisadi ili kukomesha vitendo vya rushwa.

Mwakyembe alitoa kauli hiyo jana mara baada ya kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

“Nimeulizwa sana na waandishi wa habari tangu Julai hadi sasa walitegemea kungekuwa na kesi nyingi lakini kuna kesi moja katika Mahakama ya Mafisadi tumekuja kubaini kwamba uchache wa kesi ndiyo mafanikio makubwa ya hatua ya kisheria tuliyochukua,”amesema.

Aliongeza kwa sasa waliozoea kupora mabilioni wamerudi nyuma ambapo wezi hao wameonekana wakiiba fedha chini ya Sh bilioni moja iliyopo kisheria hivyo wanategemea kujadili sheria hiyo ili iwalenge hata wanaochukua kiasi kidogo.

“Sisi kama serikali tukiona wizi sasa umenza kupungua na kuenea katika viwango vya Sh milioni 400, 500, 700 tumeanza kujadiliana kuangalia uwezekano wa kushusha kiwango cha fedha ili tuweze kukomesha kabisa udokozi, ubadhilifu, wizi wa fedha au mali ya umma,”alisema.

Aidha alifafanua uamuzi wa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda kutafuta vijana wanaojua sheria ili kusaidia wananchi kabla ya kwenda mahakamani ni mzuri.

Aliongeza kuwa tayari wamepeleka mswada wa msaada wa kisheria ambao utasaidia wananchi hasa wa vijijini na wanawake ambao ndiyo wanaumizwa na desturi zilizopitwa na muda ili kuwasaidia kupata haki na itakuwa na wasaidizi wa kisheria nchi nzima wapatao 4,900.

Makonda alisema wamejadili utoaji na upatikanaji wa haki kwa wakati kwani kuna changamoto ya watu kuwa wengi na kuchelewa kupata haki zao.

Alisema kwa kuona adha hiyo mkoa huo kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya watajenga Mahakama za Mwanzo 20 ili kuongeza kasi za utoaji na upatikanaji wa haki kwa wananchi endapo wanapopelekwa vituo vya polisi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad