Moja kati ya wasaidizi wa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa siku 22 hadi leo.
Taarifa zilizothibitishwa na ndugu zake pamoja na Chadema zimeeleza kuwa Ben Saanane ambaye ni Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa chama hicho alitoweka tangu Novemba 18 mwaka huu na kwamba hata simu zake zote hazipatikani tangu wakati huo.
Kufuatia hali hiyo, familia yake imesema iliripoti katika kituo cha polisi kilichoko Tabata jijini Dar es Salaam anakoishi Saanane na kupewa jalada lenye kumbukumbu namba TBT/RB/8150/2016.
“Kaka anafanya kazi Chadema akiwa miongoni mwa wasaidizi wa Mwenyekiti Freeman Mbowe. Ametoweka katika mazingira ya kutatanisha maana kazini wanamtafuta na nyumbani wanamtafuta bila mafanikio,” mdogo wake Ben aliyejitambulisha kwa jina la Erasto Saanane anakaririwa na Tanzania Daima.
Aliongeza kuwa wamefanya jitahada zote wakisaidiana na Jeshi la Polisi, kuangalia katika hospitali zote pamoja na vyumba vya kuhifadhia maiti jijini Dar es Salaam lakini hawakupata jibu.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vicent Mashinji alikiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa wanaendelea na jitihada za kumtafuta ikiwa ni pamoja na kuandaa utaratibu wa kichama kufahamu undani wa tukio hilo.
Hata hivyo, Kamadna wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salum Hamdun alipotafutwa na gazeti hilo alieleza kuwa ofisi yake haijapokea taarifa za tukio hilo.