MBWANA Samatta Apachika Mabao Mawili...Aongelea Kuhusu Kasi yake Kupungua


Kwa muda wa saa 15 na dakika 11, sawa na miezi mitatu, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta alikuwa kizani bila bao kutoka mguuni mwake.

Siku zote, raha ya soka ni mabao, lakini kwa Samatta, ukame wake uliodumu kwa muda mrefu ulimalizika juzi alipoiongoza timu yake, RCK Genk kuichapa Waasland-Beveren kwa mabao 3-1 katika mchezo wa Kombe la Ubelgiji, akifunga mabao mawili.

Samatta alifunga mabao hayo kipindi cha kwanza na pia jingine la Mnigeria Onyinye Ndidi yaliiwezesha Genk kusonga mbele hadi hatua ya 16 bora ya kombe hilo.

Mara ya mwisho, Samatta alifunga bao Agosti 25 kwenye mchezo wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Ulaya (Europa League) na Genk iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Lokomotiva.

Baada ya hapo, alicheza mechi 19 za ligi na mashindano mengine Ulaya bila bao na kupoteza namba kwa mshambuliaji raia wa Ugiriki, Nicos Karelis aliyeonekana kujimilikisha kwa muda namba kwenye kikosi cha kwanza.

Moja ya sababu zilizomgharimu Samatta uwanjani ni maumivu, ingawa yeye alikiri kuwa kupata upinzani mkali kutoka kwa Karelis.

“Ninayecheza naye (Karellis) anafanya vizuri, yuko kwenye kiwango kizuri, anafunga karibu kila mechi, kwa hiyo anastahili kuanza.

“Binafsi, niliathiriwa na majeraha yaliyosababisha kasi yangu ipungue, lakini nitahakikisha najituma zaidi kuanzia mazoezini hadi nirejee kwenye kiwango changu,” alisema Samatta.

Samatta anaonekana kumhofia Karelis, ingawa kwa mfumo wa soka la kisasa, anapaswa kuwachunga pia Leon Bailey na Leandro Trossard.

Samatta amefunga mabao tisa katika dakika 1,579, wakati Karelis ana mabao 14 na dakika 2,340. Trossard ana mawili na dakika 756, huku Bailey ana manane katika dakika 2,273.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad