NENO la Shukrani Kwa Wote Kutoka Kwa Mmiliki wa Jamii Forums Baada ya Kuachiwa Kwa Dhamana

Heshima kwenu wakuu!

Shukrani:

Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuiona siku ya leo nami kuwa nanyi siku hii ninapoandika waraka huu mfupi ukilenga zaidi kutoa shukrani. Shukrani hizi nilitamani nimtumie mmoja mmoja lakini nimeshindwa kwani ni wengi wanaostahili kushukuriwa.

Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine kupaza sauti zao (kwa njia yoyote ile) ili aidha nifikishwe mahakamani au niachiwe bila masharti yoyote (nilipokuwa Kituo cha Kati) na baadae kuendelea kupaza sauti kutaka mahakama initendee haki niwe huru baada ya kupelekwa gerezani Keko.

Nawashukuru mawakili wangu na wengine walioamua kujitolea kuingia katika utetezi wangu hata bila kuombwa. Kipekee, namshukuru na kumpa pole sana Ndg. Albert Msando ambaye tayari alishaonesha nia ya kuwa mtetezi wangu lakini yakamkuta yaliyomkuta, tumwombee kwa Mwenyezi Mungu apate uponyaji wa haraka.

Nipende kuwashukuru wana JamiiForums wote kwa mijadala iliyoendelea wakati wote ambao sikuwepo; vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vilivyoshiriki katika hatua hii ya awali (kazi ndio imeanza); watumiaji wa mtandao wa Twitter(bila kutaja mmoja mmoja) kwa jitihada zao ambazo zimenishangaza kuhakikisha hashtag ya #FreeMaxenceMelo ina-trend na kuwa tayari kwao kutoa maoni yao kwa vyombo vya habari pale walipohitajika kufanya hivyo; nawashukuru Wahisani mbalimbali na wadau wa maendeleo ambao walituma wawakilishi wao Central na Gerezani kufuatilia napitia maisha gani na hata kuwasiliana na mamlaka zinazohusika kutaka nitendewe haki.

Aidha, nawashukuru sana wafanyakazi wa Jamii Media ambao naelewa kwa kiwango gani kilichotokea kilivyowaathiri kisaikolojia na hata kiutendaji. Nawashukuru Asasi za Kiraia zikiongozwa na THRDC, LHRC, Sikika, C-Sema, TMF, ChangeTanzania n.k kwa kuwa mstari wa mbele kufuatilia na kuelewa kinachoendelea na hata kujitoa kwa ajili ya udhamini wangu pale walipoombwa na wengine hata bila kuombwa. Jukwaa la Wahariri(TEF) – Asanteni sana!

Nichukue fursa hii kuwashukuru pia watanzania katika makundi mbalimbali ya WhatsApp, Facebook na Telegram kwa ushirikiano waliouonesha. Watumiaji wa Instagram(nashindwa kutaja mmoja mmoja), nawashukuruni sana kwani nimeona posts nyingi toka kwa watu hata ambao hawanifahamu lakini walioelewa ninachosimamia wakitoa support kubwa sana.

Ndugu, marafiki na majirani zangu – asanteni sana kwani mlikuwa nasi bega kwa bega wakati wote. Watanzania na wote ambao si watanzania mliojitahidi kufika Central na Gerezani kunijulia hali – Asanteni sana na Mungu awabariki sana!

Kuna wale ambao hata hawajaelewa kesi inahusu nini hasa na wameanza kuwashambulia waliokuwa wakinitetea, nao nawashukuru kwani naamini ni kwakuwa hawajajua nini kimo kwenye kesi. Ila niwahakikishie kuwa si rahisi kutetea mhaini, unapoona mtu anaamua kufanya hivi ni vyema kutafakari.

Askari wa Kituo cha Kati(Central) na wale wa Gereza la Keko – asanteni sana. Naelewa ni vigumu umma wa watanzania kuelewa namaanisha nini lakini ninyi kwa andishi hili mnaelewa vema ninachomaanisha. Wengi mliifanya kazi yenu kwa weledi mkubwa.

Viongozi wa kidini(wachungaji, ma-sheikh, maaskofu n.k) na wanasiasa wote(toka vyama vya upinzani na chama tawala) mlioshiriki katika hili – Asanteni sana. Hamkuingiza itikadi za kisiasa wala misimamo ya kidini bali mlitaka haki kutendeka. Nawashukuru!

Kuhusu kesi:

Ndugu zangu, ndio kwanza kesi inaanza kuunguruma tarehe 29 Disemba 2016. Si rahisi mimi kuongelea nini kilichomo kwenye kesi lakini naamini vyombo vingine vya habari kwakuwa tunayo sheria ya Haki ya Kupata Taarifa vinajua namna ya kuhakikisha vinaueleza umma nini kilichomo ndani yake (Mahakama Kuu na Mahakama ya Kisutu) ili watanzania waweze kuelewa mbivu na mbichi. Kuna ambao watajikuta kuwa walikuwa ndio walengwa hata hawakuguswa na kukamatwa kwangu, hapo ndipo watajua tunapigania nini.

Nipende kuwaomba tuendelee kuwa pamoja katika safari hii tunayoianza. Mimi ni sampuli tu, nasimama kwa ajili ya wale ambao naamini wana haki ya kutoa maoni na kufichua maovu (ili mradi hawajavunja sheria) na ninaamini wengi tunataka haki hii isipotee na iendelee kulindwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri wa Muungano.

Sina mengi kwa leo zaidi ya shukrani.

Wenu,

Maxence M. Melo

VIDEO:TAZAMA MAAJABU YA HUYU JAMAA

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad