Hilo limethibitika baada ya kikosi cha Idara ya Uhamiaji Kanda ya Dar es Salaam kuwakamata wasichana 13, raia wa Nepal na India wanaodaiwa kufanya ukahaba kwenye madanguro wilayani humo.
Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Kanda ya Dar es Salaam, John Msumule alisema wasichana hao ambao umri wao ni kati ya miaka 18 na 20 waliletwa nchini kwa ajili ya biashara ya ukahaba.
Alisema katika operesheni ya kuwatafuta wahamiaji haramu iliyofanywa na kikosi chake, waligundua kuwapo kwa madanguro manne Kinondoni ambayo yanawatumia raia wa kigeni.
“Kinondoni ndiyo imekithiri kwa madanguro yanayowahusisha raia wa kigeni. Hili suala halivumiliki tumejipanga kuyaondoa madanguro yote.
Kazi hiyo itafanyika ndani ya siku 10, kama wahusika wanajipenda wayafunge wenyewe. Ukipita muda huo na bado madanguro yapo mje mniulize imekuwaje,” alisema Msumule.
Kikosi hicho pia kinamshikilia Mtanzania, Mohamed Magamba kwa kosa la kukutwa na hati za kusafiria za raia wa mataifa manne tofauti.
Kwa mujibu wa Msumule, Magamba hujihusisha na utengenezaji wa hati za kughushi na kugonga mihuri kwenye hati za kusafiria.
“Tumemkamata na hati za kusafiria za raia wa Nigeria, Somalia, Uingereza na Botswana. Kazi yake ni kuchukua hati za wageni, kuwagongea mihuri ya uongo na kuwatengenezea hati za kughushi,” alisema na kuongeza:
“Wahusika wa hati hizi tunawatafuta na tutawapata ndani ya siku mbili. Tunafuatilia mtandao wake kujua wanafanyaje kazi hii.”
Msumule aliwataka waajiri wanaoajiri raia wa kigeni kuhakikisha wana vibali halali kabla ya kuwaajiri.
Waajiri hakikisheni mnaajiri watu wenye vibali halali si kuchukua vibali mitaani, utaratibu wetu sasa tunawakamata raia wa kigeni wanaofanya kazi bila vibali na waajiri wao.
Pamoja na waajiri, pia Msumule amewataka wamiliki wa nyumba mkoani Dar es Salaam ambao nyumba zao zina wapangaji, kuhakikisha wanakuwa na picha za wapangaji wao wote ili kuwatambua na kupunguza uwezekano wa kuhifadhi wahalifu.
Katika ziara yake ya Novemba 15 aliyoifanya katika ofisi za Idara ya Uhamiaji hapa nchini, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, aliagiza wahamiaji wanaokiuka sheria za nchi na kuishi bila vibali, wasakwe kila kona, kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Kitendo cha mtu, ambaye si Mtanzania kuwepo nchini na kukiuka sheria na taratibu anazopaswa kuzifuata ili kuendelea kuwepo, hakuna mjadala na kwamba, akamatwe,” aliagiza.
Pia, aliagiza uongozi na watumishi wa idara hiyo nyeti, kutokumuonea mtu kwenye utekelezaji wa majukumu yao, badala yake watangulize uadilifu ili kuepuka lawama na kuchafua taswira ya ofisi hiyo.