Wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki inapenda kufafanua na kuweka sawa taarifa zilizoandikwa kwenye baadhi ya Magazeti ya tarehe 07 Desemba, 2016 kuwa mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa unakaribia kuiva na kwamba Mgogoro huo unatarajiwa kumalizwa na washauri wa kimataifa.
Taarifa hiyo haikuwa sahihi. Ukweli ni kuwa, mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwa sasa upo chini ya Jopo la Viongozi Wastaafu wa Afrika wanaotokea kwenye nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Jopo hilo linaongozwa na Mhe. Joachim Chissano, Rais Mstaafu wa Msumbiji akisaidiwa na Mhe. Festus Mogae, Rais Mstaafu wa Botswana na Mhe. Thabo Mbeki, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini.
Aidha, Jopo hili ambalo liliundwa na Umoja wa Afrika kupitia Jukwaa la Viongozi Wastaafu wa Afrika (Forum for Former African Heads of State and Government) kwa ajili ya kusuluhisha mgogoro huu, linaendelea na kazi hiyo kwa kupitia taarifa mbalimbali na maandiko yaliyowasilishwa kwao na Tanzania na Malawi. Vile vile, Jopo lilikwisha zikutanisha pande zote mbili katika mashauriano ya awali yaliyofanyika nchini Msumbiji
Wizara inapenda kuujulisha umma kuwa licha ya kuwepo kwa mgogoro wa mpaka wa Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa, mahusiano ya nchi hizi mbili yamezidi kuimarika siku hadi siku katika Nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hata wananchi wa pande zote mbili za Ziwa wameendelea kuishi kwa amani na ushirikiano wa karibu.
Aidha, katika kuimarisha uhusiano huu, Tanzania na Malawi zinatarajia kuwa na mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano mapema mwakani. Mkutano huu utawaleta watalaam wa nchi hizi mbili kutoka Sekta mbalimbali kwa lengo la kujadili changamoto za ushirikiano katika sekta hizo, kubaini maeneo mapya ya ushirikiano pamoja na kuweka mikakati ya kutekeleza miradi ya pamoja itakayokubaliwa baina ya pande hizi mbili.
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo unatarajiwa kujadili masuala ya ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, usafirishaji, fedha, nishati, utalii, ulinzi na usalama uhamiaji, uvuvi na ardhi.
Hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawaomba Waandishi wa Habari, Wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla inapohitajika kupata taarifa sahihi za suala hili kwenda kwenye Mamlaka husika na kuziandika kwa usahihi kwa ustawi wa nchi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 07 Desemba, 2016.