WELEDI wa Prof Rwekaza Mukandala Aongezewa Muda wa Mwaka Mmoja Kuongoza UDSM Baada ya Kustaafu


MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye ni Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete baada ya mashauriano ameafikiana na Rais John Magufuli kuongeza muda wa Makamu Mkuu wa chuo hicho wa sasa, Profesa Rwekaza Mukandala kwa muda wa mwaka mmoja.

Katika taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari jana, Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Peter Ngumbullu alisema uamuzi huo unaanza mara moja.

Ngumbullu alisema muda wa Profesa Mukandala ulimalizika Desemba 4, mwaka huu.

Profesa Mukandala aliteuliwa kwa kipindi cha sasa cha miaka mitano kilichoanza Desemba 5, 2011 na kumalizika Desemba 4, mwaka huu.

Profesa Mukandala alisema alikuwa tayari ameshajitayarisha kwamba juzi angekabidhi madaraka hayo kwa mtu mwingine, lakini kwa imani waliyokuwa nayo uongozi wa chuo hicho uliridhia aendelee kwa mwaka mwingine.

“Viongozi wa chuo hiki wakishirikiana na Rais John Magufuli wamekuwa na imani na mimi na kuniongezea mwaka,” alisema Profesa Mukandala.

Amewashukuru waliomchagua na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wote na jumuiya ya wanachuo ili Udsm iendelee kuwa bora. Pia alisema ataendelea kuenzi na kutunza tunu ya chuo hicho iliyoachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma (UDASA), Dk George Kahangwa alisema kuna mambo mengi Profesa Mukandala alikuwa bado anayafanyia kazi hayajakamilika, hivyo wakati anamalizia kipindi chake, ikatokea akachaguliwa mkuu mpya wa chuo hicho Kikwete.

Dk Kahangwa alisema hivyo inabidi akamilishe mambo yaliyo mezani kwake wakati wamempata mkuu huyo mpya wa chuo Kikwete.

“Hii inatoa nafasi ya kufanya utafiti mzuri ili ajaye apatikane mwenye sifa zote ambazo wahusika watakuwa wamejiridhisha,” alieleza na kuongeza kuwa wanataaluma si ajabu mtu akastaafu lakini akaongezewa muda kutokana na umuhimu wanaokuwa nao.

Alisisitiza kwao wanajumuiya ya chuo hicho lililo la muhimu ni Profesa Mukandala kuwapatia Chuo Kikuu wanachokitaka. Naye Rais wa Serikali ya Wanachuo Udsm (Daruso), Leon Erasmi alisema amefurahishwa na hilo kwa kuwa Profesa Mukandala amekuwa na ushirikiano mzuri na wanafunzi.

“Mukandala amekuwa ni kiongozi mzuri tumejifunza mengi kutoka kwake. Ofisini kwake wanafunzi kumuona ni muda wowote pia amekuwa akishughulikia changamoto tulizonazo au kutuelekeza kwa mtu mwingine huku akifuatilia kwa ukaribu,” alieleza Erasmi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad