SIKU moja baada ya kutokea kwa moto katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano imeunda timu ya watu 12 kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha
moto huo.
Moto ulizuka juzi majira ya saa tano usiku katika chumba cha
kuhifadhi mizigo kwenye jengo namba mbili (terminal II) na kuteketeza
mizigo yote iliyokuwamo katika chumba hicho kidogo.
Tume hiyo imeundwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa ambaye alifika katika uwanja huo majira ya saa
sita mchana akitokea mkoani Mwanza na kwenda moja kwa moja katika chumba
hicho kilichoteketea ili kuona uharibifu uliojitokeza.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo, Mbarawa alisema, baada ya
kutokea kwa moto huo hatua za haraka za kuuzima zilichukuliwa na kwamba
wakati moto huo unatokea hakukuwa na mtu yeyote katika eneo hilo ambaye
amedhurika.
Alisema baada ya kuzimwa kwa moto huo hatua ya pili ili kuwa ni
kurejesha huduma ambapo walihamisha huduma kutoka katika jengo hilo
kwenda katika jengo namba moja (terminal I) kwa kuwa kulikuwa na ndege
ambazo zilikuwa uwanjani hapo.
“Tuliendelea kupeleka huduma zetu katika jengo la abiria namba moja
na huduma ikaendelea kama kawaida, kwanza tulizima moto lakini pia
tukawa tunaendelea na huduma kule. Huduma ziliendelea kule na wakati huo
huo tukaja huku kutayarisha mifumo mingine kuhakikisha jengo hili
liweze kutoa huduma muda mfupi baadaye,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema jambo la tatu ni kutafuta chanzo cha moto kwa kuwa moto
hauwezi kutokea bila kuwa na sababu ya kitaalamu, hivyo timu hiyo
itafanya kazi ya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha moto huo.
Alifafanua kuwa timu hiyo itafanya kazi kwa muda wa mwezi mmoja na
itaoa majibu ya uhakika ya chanzo cha moto hiyo ambayo itasaidia kuweka
mikakati ambayo itazuia matatizo ya moto katika viwanja vya ndege vyote
nchini. “...ni timu ambayo ina watu wenye uwezo na ujuzi, ninaamini
watatupa majibu ya uhakika, hawataupa majibu ya bahati mbaya ilitokea,
kwenye utaalamu hakuna kitu bahati mbaya kuna sababu ya msingi,
nategemea kupata ripoti ya kitaalamu inayosema chanzo ni nini,” alisema.
Alisema baada ya kupata ripoti hiyo wataweka mikakati ya kuzuia
majanga ya moto katika viwanja vyote vya ndege nchini ili tukio hilo
lisijirudie tena. Alisema kuwa kwa sasa hawawezi kumnyooshea mtu kidole,
kwa kuwa kuna sababu ya kitaalamu.
Tume hiyo inaongozwa na Joseph Nyahende kutoka Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA) imepewa kazi ya kutoa taarifa ya sababu za moto
huo.
Hadi sasa thamani ya mizigo hiyo bado haijafahamika.
Moto huo ulizuka katika chumba kidogo kinachotumika kuhifadhia mizigo
ya abiria wanaotoka nje ambayo huhifadhiwa hapo kutokana na mmiliki
wake au mzigo huo kuchelewa kufika, inayohudumiwa na kampuni ya
Swissport ambao ni wasimamizi wa mizigo yote inayopitia katika uwanja
huo wa ndege.
Download Application ya Udaku Special Blog Kwa Kubonyeza Hapa