DAR ES SALAAM: Mkongwe wa muziki wa kizazi kipya wa Uganda,
Joseph Mayanja ‘Jose Chameleone’ amejipatia zaidi ya shilingi milioni
100, mali ya mzalishaji nguli wa muziki wa Bongo Fleva, Paul Matthysse
‘P Funk’,
Chameleone anadaiwa kuuza mdundo (beat)
mali ya P Funk bila kumpa hata ‘thumni’ na yeye kutia kibindoni zaidi ya
dola 50,000 za Kimarekani, (zaidi ya shilingi milioni 100) baada ya
kulipwa na kampuni inayojishughulisha na masuala ya filamu, Walt Disney
ili kuruhusu mdundo unaosikika katika kibao cha Profesa Jay cha
Nikusaidieje, mali ya P Funk, utumike kwenye sinema ya Queen of Katwe
iliyotoka mwishoni mwa mwaka jana bila ridhaa yake.
Akizungumzia sakata hilo, P Funk
alisema, Chameleone si mtu mzuri kwani alianza kumuingiza mjini tangu
mwaka 2006 alipoichukua beat ya Nikusaidieje na kuiingizia mashairi ya
wimbo wake na kuuita Bomboclat.
“Unajua zamani tulikuwa tunatoa wimbo
katika mfumo wa CD, tunapeleka redioni. Kwenye hiyo CD tulikuwa tunaweka
beat tupu, sauti pekee (akapela) na wimbo wenyewe uliokamilika.
“Sasa jamaa (Chameleone) akaiba ile beat, akaingiza mashairi ya
Bomboclat bila hata kuniambia chochote. Nikamueleza, akakubali kunilipa
dola 2000. Nikamkubalia lakini akaingia mitini. Kama hiyo haitoshi,
wimbo huohuo ambao beat yake ameniibia, akaenda kuuza tena Walt Disney,
napo nilimcheki akaanza kuleta longolongo zilezile za mwanzoni.
“Akaanza ooh sijui nimefanya ili tuzidi
kujitangaza mara ooh sijui wamenipa hela kidogo kama dola 2000, nikaona
huyu anataka kuniletea ushenzi, lazima nimfunze adabu, nikazungumza na
Cosota (Chama cha Hakimiliki Tanzania), wakawaandikia barua wenzao wa
Uganda lakini nao hawakujibu chochote,” alisema P Funk.
Ili kumuonesha kwamba ‘amemaindi’, P
Funk kupitia kwa wanasheria wake waliuandikia barua ya kiofisi (official
letter) uongozi wa Disney ambao ulishtuka kusikia kwamba yeye ndiye
mmiliki halali wa mdundo huo, hivyo ukamuomba suala hilo walimalize
kirafiki.
“Wameniambia kwamba watafanya mahesabu
yao na kuona natakiwa kulipwa kiasi gani na wao wenyewe watajua
Chameleone watamshughulikia vipi,” alisema P Funk.
Risasi Mchanganyiko lilifanikiwa kupata
simu ya nyota huyo mkongwe wa Uganda, lakini baada ya kujitambulisha na
kumsomea tuhuma hizo, alisema yeye siyo Chameleone, bali ni mtu wa
menejimenti yake ambaye alipotakiwa kutoa majibu ya kiofisi kuhusu suala
hilo, alisema mwenye majibu ni msanii mwenyewe.
Mtu huyo wa menejimenti alitoa namba
binafsi ya mwimbaji huyo wa kibao cha Valuvalu, lakini mara zote kutwa
nzima jana, kila alipopigiwa, simu yake iliita bila kupokelewa hadi
ilipokatika.
Licha ya kutumiwa pia ujumbe uliojaa tuhuma hizo, Chameleone hakujibu.