Askofu Mokiwa aliyasema hayo kwenye Kanisa la Anglikana Ilala jana, alipozungumza na waandishi wa habari. Alisema licha ya kusemwa mambo magumu, lakini yeye kama Askofu, kazi yake ni kuwaombea waliomkosea na hana matatizo nao, kwani amekwisha wasamehe.
Askofu Mokiwa pia alienda mbali zaidi kwa kudai kuwa Dayosisi ya Anglikana Dar es Salaam haina mgogoro, bali viongozi watano wa dayosisi hiyo ndio wanatengeneza mgogoro huo kwa maslahi binafsi, wakitumia Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Andrea la Magomeni kama njia ya kupitishia migogoro yao.
“Siogopi kusema baba askofu kapotoka katika hili, ameshauriwa vibaya na washauri wake wa kisheria,”alisema Askofu Dk Mokiwa ambaye alimtaja Profesa Palamagamba Kabudi kuwa mshauri wa kisheria wa askofu mkuu.
Kauli hiyo ya Mokiwa imekuja siku chache baada ya kuvuliwa uaskofu, kwa kile kilichoelezwa mashtaka 10 yaliyofunguliwa na walei 32 wa Kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam, yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa, ndio sababu ya Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Jacob Chimeledya kumvua uaskofu.
Hata hivyo, Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo, kwa maelezo kuwa mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Saalam, ambayo ndiyo yenye uamuzi wa kumfuta kazi na si askofu mkuu; au askofu mwingine yeyote wa kanisa hilo Tanzania.
Uamuzi wa kumvua uaskofu, ulichukuliwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Askofu Chimeledya baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu, kama ilivyoshauriwa na Nyumba ya Maaskofu, ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji, ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini.
Akizungumzia suala hilo, Mokiwa alisema, “Alikuja na maaskari zaidi ya 12 ambao wamevaa sare, na wengine ambao hawakuvaa sare sijawajui idadi yake, askofu mkuu alidai amekuja kuleta mrejesho wa halmashauri kuu, na matokeo yake akaishia kusema ameniondoa kwenye huduma ya uaskofu.
"Nimesema siondoki, na nimeona wanasema wataweka kila kitu hadharani, nawambia hivi, mimi ni msafi na sina uchafu sehemu yoyote ile, wawe huru na amani kuanika madudu yangu kama yapo, waweke tu hadharani wala siogopi.
“Ninavyo vyombo halali kwenye Dayosisi hii ambayo hakutaka kukutana navyo ambavyo ni Halmashauri ya Kudumu, hakuwahi kutaka kuwasiliana na sisi, sisi tulitaka kuwasiliana na yeye, angejibu mawasiliano yetu ya kujenga mahusiano na kutekeleza yaliyoamuliwa, hukutaka kutekeleza leo unakuja na hoja ya kuniaondoa.
“Halmashauri ya Kudumu inamwambia hatujawahi kumpelekea mgogoro sisi kama Dayosisi ya Dar es Salaam, waswahili wanasema ‘jipu linamsumbua mwenye mwili wake’, hujawahi kupelekewa neno lolote la machafuko, ni nani aliyekwambia Dayosisi ya Dar es Salaam ina migogoro?
“Askofu anafanya kazi na sisi, askofu ana vyombo vya kutawala, hana mamlaka ya kujiamulia mambo yake mwenyewe, ukisema Dar es Salaam kuna machafuko wewe Askofu Mkuu tunajua unasimama na watu na makundi katika Dayosisi hii.
“ Yeye ni askofu kama mimi, yeye yupo Mpwapwa, tuna taratibu zetu kama za bendera ukiingia mahali unashusha bendera kidogo, kwa nini Askofu Mkuu afanye kazi na watu ambao sio sehemu ya mamlaka ya Dayosisi ya Dar es Salaam.
“Halmashauri Kuu inamwambia kwa kuwa amekuja na tamko lake bila ya kuwashirikisha, wamemwambia Dar es Salama kuna askofu mmoja tu ni Mokiwa.
“Yeye kama Askofu Mkuu hakupaswa kucheza nje ya Nyumba ya Maaskofu, mimi pia naingia kwenye Nyumba ya Maaskofu, kuchomoka na kufanya kazi nje ya taratibu, hii sio sawa.
"Askofu Mkuu ana timu yake ya maofisa ambao wamemshauri vibaya, na yote yaliyonukuliwa yote yamekosewa katika kusimamia taasisi, kila taasisi ina uhuru wa kurekebisha pale palipoharibika pasipo kuingiliwa.
“Dayosisi ya Dar es Salaam haina mgogoro na mimi ndio Askofu wake, mgogoro uliopo ni wa kutengeneza, katika timu yake kuna watu wenye ‘interest maalum’ ambao ni Profesa Palamagamba Kabudi, yeye ndio mshauri mkuu wa askofu lakini amekuwa akimpotosha, askofu akikosea na yule ni mwanasheria aliyebobea na ndiye anayeingiza kanisa kwenye migogoro iliyobobea.
“Tumewahi kuandikiwa barua na serikali Kanisa letu ndio vinara wa migogoro, wamekuwa wakitengeneza mgogoro kati ya waumini na maaskofu wasielewane, wakubwa waingie kushika hatamu za uongozi hapa.
“Nina kibali cha kuzungumzia Dayosisi ya Victoria Nyanza Mwanza, uongozi wa kanisa umeingia pia na kufanya kazi na makundi, kando ya taratibu, kugombanisha askofu na watu wanaowangoza na kusababisha maumivu makubwa, lakini nasema bila kufuata taratibu yeye akiwa kiongozi mkuu, ni hatari sana kiongozi anayeacha kuongoza kwa taratibu na kufuata matakwa yake mwenyewe. "
Ataja majipu 5 ndani ya Kanisa
Askofu Mokiwa alisema kuwa ndani ya Kanisa hilo, kuna majipu ambayo yamekuwa kiini cha migogoro kila kukicha na kuchafua taswira nzima ya kanisa hilo.
“Askofu Mkuu anashauriwa na Mwanasheria (Profesa Kabudi) anayeheshimiwa na watu wengi, aliyezalisha wanasheria wengi zaidi katika nchi hii lakini halitendei haki kanisa, halisaiidi kusimama sawa sawa, kuliokoa kanisa na mvurugiko, haonekani mara zote kwa kuwa amejificha nyuma ya taratibu hizo.
“Mwingine ni askofu Oscar Mnung’a, Makamu Askofu Mkuu, huyu anakuja kufanya kazi na makundi Dar ili aje kuwa askofu mkuu, alikuwa padri wangu na ni askofu wa Newala, naamini watu wa Mpwapwa na Newala wanawafahamu, kuwa ndio viongozi wao ndio chanzo cha maumivu kwenye kanisa hili.
“Mwingine ni Johnson Chinyong’ole ni Katibu Mkuu, Padri wa Dayosisi ya Morogoro, moyoni mwake anaamini mimi ndiye niliyebana asiwe askofu mkuu, nataka kusema Kanisa Anglikana ni Kanisa kubwa nchi hii, alipaswi kuonekana na dalili yoyote ya migogoro, lina uwezo wa kufanya mambo yake ndani bila ya kuvuana nguo kama ilivyo sasa tena bila ya sababu za msingi.
“Askofu mkuu anafanya kazi na Kanisa la Andrea Mtakatifu Magomeni, kule kuna mtu anaitwa John Mhina, yule alikuwa Padri katika dayosisi yangu na tulimuondolea haki za sakramenti na huduma za kichungaji mikononi mwake, tulifanya hivyo kwa sababu ya kukiuka jambo moja tu la utii.
“Tulifanya uhamisho katika Dayosisi ya Dar akagoma, akatengeneza tuhuma kwa taasisi moja kubwa ambayo naiheshimu, na sitaki kukosea ikavurugikiwa kwa sababu ya maneno ya kinywa changu, taasisi hiyo sina uchafu nao, na sina uchafu popote.
“Sababu ya Mhina kumuondoa ni kwamba haifai, mtu ni kuhani wa Mungu halafu anaenda kukopa benki na kukimbia vielelezo ninavyo, benki alizokopa ni BOA, Akiba Commercial Bank na Tanzania Investment ambayo iliwahi kumtoa mpaka picha zake.
“Mwingine ni Paul Mtweve alikuwa mkuu wa idara ya Uinjilisti, naye nilimuondoa kwa sababu za kiuaminifu, kulikuwa na Saccos ambayo alijikopesha na sasa imefungwa, wamechafua taswira nzima ya Dar es Salaam na ndio wamekuwa wakitumika na askofu mkuu, ndio wamekuwa vinara wa kutengeneza mashaka. Kuthibitisha kuwa wanafanya kazi na Askofu mkuu, uhamisho wa Mhina, alipopinga kuhama, askofu Mkuu ‘alisapoti’, kwangu mimi kwa Dar es Salama sio tena Askofu, mwaka jana sikukuu ya Matende alisema amehamina Mpwapwa sasa sijui amebaki huko au vipi maana hapa sijamuona.
“Nilisali Ubungo siku ya Krismasi, e-mail zilinaswa ambazo zilikuwa zikisambazwa kwa wanangu wa Magomeni ambao hawakusali Krismasi kwa sababu walipewa taarifa kupinduliwa kwangu, hivyo walijua kutakuwa na mapinduzi.
“Taasisi za dini hazipaswi kufanya kama hivi ni aibu, waumini wakimbilie wapi wakati wanaamini Kanisa ndio mahali salama.
“Waumini watulie, kwa jimbo la Dar es Salaam hawatatusikia katika migogoro yoyote, bado nina imani na waumini wa Dayosisi hii, tushikane pamoja, kuifanya kazi ya Mungu.
“Tuna shule, vituo vya watoto yatima, nataka ninaofanya nao kazi bila njaa, na wale wanaocheza nje ya zizi, warudi kundini nitawakaribisha,” alisema.
Mokiwa alifunguliwa mashtaka 10 Machi 2015 ambayo ni kuizuia dayosisi ya Dar es Salaam, kupeleka michango pasipo maelekezo ya Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, kuhamasisha dayosisi kujitoa katika udhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania (KAT) kwa lengo la kuifarakanisha dayosisi na Jimbo, kinyume na katiba ya dayosisi.
Mashitaka mengine ni kufuja mali za kanisa na kuingia mikataba kiholela yenye viashiria vya rushwa katika eneo la kanisa la Mtoni Buza na miradi mingine, kushindwa kutatua migogoro inayohusu uwekezaji na maadili baina ya dayosisi na mitaa ya Magomeni ambao kuna mgogoro na Benki ya DCB, kanisa la Kurasini na mengine.
Askofu huyo pia anadaiwa kushindwa kutatua migogoro baina ya mapadiri na waumini na kutunza mali za kanisa katika mtaa wa Watakatifu wote Temeke na kutelekeza nyumba ya askofu iliyopo Oysterbay ambako imegeuzwa kuwa yadi ya kuuza magari.
Pia alilalamikiwa kushitakiwa mahakamani na Marehemu Christopher Mtikila na watu wengine watatu kwa kosa la kuwatishia silaha ya moto na kuwapapasa maungoni mwao bila ridhaa yao kinyume na maadili ya kikanisa.
Askofu Mokiwa pia analalamikiwa kuanzisha taasisi ya MEA Foundation iliyomwezesha kupokea fedha nyingi za wafadhili kwa ajili ya maendeleo ya dayosisi, lakini fedha zimefujwa na hesabu za chombo hazikuwahi kukaguliwa.
Tuhuma zingine ni kurejea kwa mchakato wa mapitio ya katiba mpya na kuvuruga mchakato wa awali wa maandalizi ya katiba mpya ya dayosisi kwa kutumia fedha za dayosisi na kutekelezwa askofu msaidizi dayososi ya Katanga Kalemi .
Hata hivyo akijibu tuhuma hizo Mokiwa alisema; Nyumba ya Maskofu Oysterbay
“Ile nyumba haijatekelezwa bali vigae vilikuwa vinaanguka, nina kijana wangu ambae ana matatizo mpaka sasa ni mkubwa lakini hasemi vizuri kuna siku nilimkuta anacheza na nyoka, paa linavuja mvua zikinyesha, ndio niliamua kuhama na sasa naishi nyumbani kwangu Mbezi Luisi.
“Kuna fedha Sh milioni 60 ambazo zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa nyumba hiyo ikikamilika nitarudi kukaa.
“Silverhok iliyopo Upanga, nyumba haikuwa kwenye hali nzuri jengo halikua salama, ndio maana tuliwahamisha na jengo halijatekelezwa kwani tunataka kulifanya la kisasa kama majengo mengine yanayozunguka eneo lile la Mindu.
"Fedha za DCB Kuna watu wanaeneza nimekuwa nikilipwa Shilingi bilioni 6 na DCB, huku ndani mimi nimewahi kuunda chombo ambacho kinahusisha DCB Magomeni, wa wawakilishi wa dayosisi, lakini Magomeni wenyewe ndio wanakimbia vikao, DCB ndio waliojenga na ndio wanaolipa Kanisa Dayosisi ya Anglikana.
“Kama ni vita yenye maslahi, fanyeni uchunguzi mjue anayepokea fedha kutoka DCB ni nani, mtapa ukweli kuwa ni Magomeni wenyewe, inashangaza wao ndio wanakula na kushiba lakini ndio wamekuwa wakipiga kelele na kupotosha watu.
“Kwa mikono yangu niliwaidhinishia Sh milioni 200 za ujenzi wa Kanisa lakini mpaka leo halijajengwa, mabati yapo pale yamesimama kama kaburi, hakuna kilichofanyika na hela zimeliwa, waseme yote kwa ukweli na sio kuweka siasa. "