Mvutano wa uongozi katika Kanisa la Anglikana, umechukua sura mpya baada ya Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Jacob Chimeledya kutishia kuweka hadharani nyaraka zinazoonyesha ubadhirifu anaodaiwa kufanya Askofu wa Kanisa hilo Jimbo la Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa, endapo ataendelea kung’ang’ania madarakani.
Dk Chimeledya alibainisha kuwa iwapo Dk Mokiwa ataendelea kung’ang’ania madarakani, ataweka hadharani mambo ambayo alidai asingependa waumini wake wala Serikali kuyajua kwa ajili ya kulinda heshima ya kanisa hilo.
Wakati Askofu Chimeledya akiyasema hayo, Askofu Mokiwa amesema atazungumza na wanahabari leo kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo dhidi yake.
Msemaji wa Askofu Mokiwa, Yohana Sanga alisema atazungumza na kujibu maswali yote ambayo wengi wametaka kuyajua kutoka kwake baada ya kuamuriwa kujiuzulu.
Awali, Askofu Chimeledya alimuamuru Askofu Mokiwa kujiuzulu kwa kile alichodai amevunja misingi ya kanisa.
Jana, Askofu Chimeledya aliwataka waumini wa kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam kuacha kulalamika kwani askofu wao hakuonewa.