UONGOZI wa Simba umesema unafanya mpango wa kumrejesha kikosini
mshambuliaji wake wa zamani Emmanuel Okwi aliyevunja mkataba na klabu ya
Sonderjyske ya Denmark.
Taarifa za kwenye mtandao wa klabu hiyo juzi ziliandika kwamba Okwi
amefikia makubaliano ya kuvunja mkataba baada ya kukosa nafasi ya
kucheza kwenye kikosi hicho.
Jana jioni Ofisa habari wa Simba, Haji Manara aliandika kwenye kurasa
zake za mitandao ya kijamii: “Kocha Omog (Joseph- kocha mkuu wa Simba)
ikimpendeza, Emmanuel Okwinho (Okwi) dimbani Feb 18, hiyo ndio habari
mpasuko, ukinuna ongeza limao,”.
Simba inatarajia kucheza na Yanga katika mechi ya raundi ya pili ya
Ligi Kuu baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza.
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Manara alikiri kuwa
uongozi wake uko kwenye mchakato wa kumnasa mchezaji huyo na ikiwezekana
atumike kwenye mechi zilizosalia za Ligi Kuu.
“Ni kweli tutamsajili kama mchezaji huru,” alisema.
Hata hivyo, tayari dirisha dogo la usajili kwa klabu za ligi
limeshafungwa mpaka msimu ujao. Akilizungumzia hilo, ofisa habari wa
Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema Simba haiwezi
kumtumia Okwi kwa sababu dirisha la usajili limeshafungwa.
“Ingewezekana kama usajili wa dirisha dogo ungekuwa haujafungwa,
lakini dirisha limeshafungwa hivyo kama wanataka kumtumia, wasubiri
mpaka usajili mwingine,” alisema.
Wakati wa usajili wa dirisha dogo Desemba mwaka jana Simba ilitaka
kumsajili mshambuliaji huyo Mganda lakini ilishindwa baada ya klabu ya
Sonderjyske kutaka ilipwe karibu sh milioni 240.
Hasimu wa Simba, Yanga pia ilijaribu kutaka kusajili mshambuliaji
mwingine ili ashindane na Donald Ngoma baada ya kudaiwa kugoma kucheza
kwenye mechi za kombe la Mapinduzi lakini ilishindikana kwa vile dirisha
la usajili lilishafungwa.
Sonderjyske ilimsajili Okwi Julai 2015 kutoka Simba kwa mkataba wa
miaka mitano uliotakiwa kumalizika mwaka 2020 ambapo tangu amesajiliwa
Okwi alicheza mechi nne tu za Ligi Kuu ya Denmark na mbili za kombe la
DBU ambapo alifunga mabao mawili.
Simba pia iliwahi kumuuza Okwi Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka 2013
kwa dola za Marekani 300,000 kabla ya kusajiliwa na Yanga alipocheza kwa
muda mfupi na kurejea Simba.
Okwi ni mshambuliaji kipenzi cha wanasimba kutokana na mafanikio
aliyoipatia timu hiyo ambapo jana baada ya Manara kuweka suala lake
kwenye mitandao ya kijamii, karibu mashabiki wengi wa soka walikuwa
wakimzungumzia.
Mmmmh hawa viongozi wa simba hawajiulizi kwa nini Sonderjyske hawakuwa wanamtumia?Hivi inawezekana mchezaji mzuri na nidhamu safi asipate namba kweli?Tatizo la simba Viongozi ndio wanamtaka Okwi,tunarudi tena kulekule kwa kutaka kumfunga Yanga tu ubingwa tuusikie kwa wenzetu,sio vyema kabisa.Mna uhakika gani kama Okwi yule ndio Okwi wa sasa ukizingatia alikuwa hachezi?Tutaendelea kutafuta mchawi wakati mchawi tunatembea nae,tuna wimbo yanga wanabebwa wakati ukiangalia makosa yanayowafanya yanga waonekane kubebwa na simba yapo.Wachezaji wa Yanga na viongozi wao kwa sasa wametulia,wako kimya hadi raha,angalia kwetu sasa mipasho utadhani waimba taarabu,hakuna nidhamu kabisa.Fanyeni kama wasomi bhana,mashabiki tumeumia vya kutosha.
ReplyDeleteWA KAZI GANI?HIVI HAKUNA MWINGINE MPAKA MNARUDISHA OKWI MARA MBILI TATU MSIMBAZI?
ReplyDeleteHAHAHAHAHA MMEKURUPUKA,HAWEZI KURUHUSIWA KUCHEZA USAJILI USHAFUNGWA AU KIGEZO GANI KITATUMIWA?BASI KAMA HIVYO NA WENGINE WARUHUSIWE KUSAJILI.
ReplyDelete