BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) imeendelea kufuatilia waajiri wasiotekeleza sheria ya bodi ya kuwataka kupeleka makato ya wanufaika wa mikopo waliopo katika ofisi katika taasisi na kampuni mbalimbali Dar es Salaam.
Katika ufuatiliaji huo, jana bodi hiyo ilikwenda katika kampuni tatu, Kampuni ya ndege ya Precision, Kampuni ya Mantrac na kampuni ya vinywaji baridi ya Pepsi (SBC Tanzania Limited ).
Wakiwa katika ofisi za Precision, walishindwa kuonana na uongozi baada ya katibu muhtasi kukataa kutoa ushirikiano kwa madai hawakuwa na miadi na uongozi wa kampuni hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo wa HELSB, Phidelis Joseph alisema, amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na Precision.
Alisema licha ya kampuni hiyo kugoma kutoa ushirikiano, lakini wamekuwa na tabia ya kulimbikiza marejesho, jambo ambalo sio sahihi na kupeleka baadhi ya majina huku mengine wakiyaacha.
“Leo (jana) tumekosa ushirikiano wamegoma kuonana na sisi, kampuni hii ni moja ya ambazo zimekuwa na usumbufu na kushindwa kuleta marejesho kwa wakati wanapaswa kulipa Sh milioni saba kwa mwezi wameshindwa kufanya hivyo na kusababisha kuwa na deni la Sh milioni 31 kama faini kwa kuchelewa kupeleka marejesho kwa kipindi cha miezi 20,” alisema.
Aidha alisema idadi iliyotolewa na kampuni hiyo ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watumishi katika kampuni hiyo ambayo vyanzo vya bodi hiyo imebaini uwepo wa wanufaika wengine katika kampuni hiyo lakini majina yao hayajapelekwa na mwajiri katika bodi hiyo.
“Haiwezekani kampuni kama Precision iwe na wanufaika saba tu shirika zima, sisi tunatambua wapo zaidi ya hao saba tunachokitaka walete majina ya wanufaika wote na pia walete marejesho kwa wakati ili fedha hizo zitumike kwa wanafunzi wengine wanaohitaji kupata mkopo na kama wakishindwa kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria,”aliongeza.
Akiwa Pepsi, Joseph alisema, kampuni hiyo imekuwa ikisumbua kwa muda mrefu, kwani wametengeneza bili ya watu zaidi 45 waliorodheshwa kama wanufaika tangu Septemba mwaka 2015, lakini hawajapeleka fedha na kila mara wamekuwa wakiwasiliana na kiongozi wa kampuni hiyo, lakini amekuwa akionesha dharau bila kutoa ushirikiano, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
“Tunashangaa hapa makao makuu hawaleti fedha hizo lakini katika matawi yao ya Moshi na Arusha wamekuwa wakilipa tunataka leo wamtume mtu ofisini kwetu kuchukua majina ambayo tumeyaorodhesha na majibu ya kwanini wameshindwa kulipa kwa muda mrefu pamoja na majina halali ya wanufaika na wakishindwa tutawachukulia hatua,”alisema.
Katika Kampuni ya Mantrac, Joseph alisema kampuni hiyo imeonekana kuorodhesha majina machache, ili hali vyanzo vya bodi hiyo vinafahamu uwepo wa wanufaika wengine wanaofanya kazi hapo.
Pia alisema kampuni hiyo imeshindwa kulipa marejesho tangu mwezi Julai mwaka jana, hivyo amewataka kuhakikisha wanalipa malimbikizo hayo kwa wakati ili kuepuka faini.
“Tumezungumza na Meneja rasilimali watu na tumemueleza ameahidi kufuatilia na kuhakikisha wanaleta marejesho ambayo wameyalimbikiza kwa wakati na kufuatilia kuona kama kuna wanufaika zaidi walioajiriwa lakini majina hayajatufikia,”aliongeza.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa bodi hiyo, Wambura Mkono alisema, waajiri wanatakiwa kuwasilisha majina ya wafanyakazi wao ndani ya siku 28 baada ya kuwaajiri ili waweze kuwaangalia endapo ni wanufaika au la; na atakapojulishwa kuwa ni wanufaika, anatakiwa kumkata asilimia 15 ya mshahara wake na kuiwasilisha bodi ya mkopo kabla ya tarehe 15 ya mwezi unaofuata katika kalenda.