Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameeleza sababu ya kupanda kwa bei ya
vyakula masokoni, na kusema hali hiyo inasababishwa na uhaba wa chakula
katika nchi jirani
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo mjini
Dodoma na amekiri baadhi ya mazao katika masoko yamepanda bei kutokana
na uhitaji wa nchi za jirani zikiwamo za Afrika Mashariki kama Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Kenya, Somalia na Sudan ambazo
zinategemea kupata chakula kutoka Tanzania.
Pia amesisitiza kuwa nchi haijakumbwa na
baa la njaa huku amewataka Watanzania utosikiliza kampeni za
upotoshwaji zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiasha kuhusu hali ya
chakula kwani si za kweli bali ni za uzushi zenye lengo la kupandisha
bei za vyakula.
“Mwaka jana nchi ilikuwa na akiba ya
chakula cha zaidi ya tani milioni tatu hali iliyopelekea baadhi ya
Wabunge na wafanyabiashara kuomba kibali cha kuuza nafaka nje ya nchi,
ambapo Serikali ilitoa kibali hicho baada ya kujiridhisha kuwepo kwa
akiba ya kutosha ya chakula,” amesema.
Amesema baada ya kutolewa kwa kibali
hicho tani milioni 1.5 ziliuzwa nje ya nchi na kiasi cha tani milioni
1.5 zilizobaki zilihifadhiwa kama akiba ambapo tayari wameruhusu ziuzwe
hapa nchini ili kupunguza kupanda kwa bei za vyakula nchini.
“Naomba wananchi msiwe na wasiwasi juu
ya hali ya chakula nchini. Msisikilize kelele zinazopigwa na watu
mbalimbali pamoja kwenye baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo magazeti
kwani taarifa hizo si za kweli. Chakula kipo cha kutosha licha ya mvua
kusuasua katika baadhi ya maeneo nchini,” amesema.
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa kwa
sasa mvua zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo
amewaomba wananchi kuzitumia kwa kulima mazao ya muda mfupi
yanayostahimili ukame.