CHAMA Cha Mapinduzi (CCM)
kimewaangukia Watanzania kwa kuomba msamaha kutokana na makosa
yaliyojitokeza kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.
Msamaha
huo umeombwa Dar es Salaam juzi usiku na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Humphrey Polepole, alipozungumza katika kipindi cha ‘Mada Moto’
kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Channel Ten.
Akiwa
katika kipindi hicho ambacho mada ilikuwa ‘Mwaka mmoja wa Serikali ya
CCM’, Polepole pamoja na mambo mengine, alizungumzia pia mwelekeo wa CCM
kwa miaka 40, itakayodhimishwa Februari 4, kwa kusema kuwa ilifikia
hatua baadhi ya wananchi walivunjika moyo kutokana na matendo ya chama
hicho.
“Chama
Cha Mapinduzi kimejifunza sana katika hii miaka 40, lakini kabla ya
uchaguzi wa mwaka 2015, inawezekana kabisa tumekosea sana na kweli
ilifika pahala wananchi walivunjika moyo kwa baadhi ya matendo
tuliyoyafanya, na mimi kama kiongozi nabeba dhamana ya wote,
watusamehe,” alisema.
Pasipo
kufafanua zaidi makosa yaliyojitokeza kabla ya uchaguzi huo na kufikia
hatua hiyo ya kuomba msamaha, alisema CCM ni sikivu na kwamba ilisikia
pale Watanzania waliposema igeuke.
“CCM
ni sikivu, kimesikia pahala ambapo Watanzania walituambia geukeni hapo,
na uongozi wa awamu ya tano, chini ya CCM na uongozi wa chama chetu
chini ya uenyekti wa Dk. John Magufuli, Makamu wa Mwenyekiti Bara na
Zanzibar, Katibu Mkuu Kinana (Abdulrahman), Naibu Katibu Mkuu Bara na
Zanzibar na sisi katika sekretarieti na pia vikao vyote vya chama,
mkutano mkuu, Halmashauri Kuu, Kamati Kuu walifika wakasema imetosha,
hatuwezi kuendelea kutosikiliza sauti za Watanzania. CCM si tu
kinapendwa na wanachama, bali na umma wa Watanzania,” alisema Polepole.
Hata
hivyo, Polepole katika kipindi hicho alisema baada ya kujitazama ndani
ya CCM wameamua kutumia msingi wa kujikosoa, kujisahihisha na kwamba
imekuwa desturi ya chama hicho kuja na mageuzi makubwa yanayotazama
maeneo matatu.
Polepole aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na mageuzi ya kiuongozi kwa kutaka chama hicho kiwe cha mfano.
“Tunataka
kiongozi wa CCM ukimtazama unasema huyu ndiye. Ni mwadilifu, ni
mwaminifu, mchapakazi, anapiga vita rushwa, ni mkweli, anaamini katika
haki, usawa na mambo yanayofanana na hayo,” alisema na kuongeza:
“Ni
mtu ambaye kwa hakika miongoni mwetu ni bora kuliko sisi, huyu ndiye
kiongozi wa chama, mzalendo wa kweli anayejiweka yeye nyuma na kuweka
wengine mbele. Si mbadhirifu, mnyenyekevu, si mwenye mwenendo usiofaa,
hayo ndiyo mageuzi ya CCM.”
Polepole
alisema licha ya sifa hizo, hata mtindo wa kiuongozi ni shirikishi
unaosikiliza wanachama ili kukirejesha chama kwa wanachama.