SERIKALI ya China imeisifu Tanzania kwa kuzingatia sera ya uwazi katika ushindanishaji wa zabuni za miradi ya ujenzi, ikilinganishwa na nchi nyingine zilizopo katika ukanda wa Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki.
Hayo yamesemwa hivi karibuni mjini hapa na Mwenyekiti wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya CRJE ya nchini China, Hu Bo wakati akizungumza na waandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni ya Taifa ya nchi hiyo (CCTV) waliofika nchini kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali yao nchini Tanzania.
Mwenyekiti huyo alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazoongoza kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu za zabuni za ujenzi, ambapo Serikali ya Tanzania imekuwa ikitoa kipaumbele kwa makampuni ya ukandarasi ya wazawa kwakukubali maombi yao ya zabuni za ujenzi.
“CRJE inafanya shughuli zake katika mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda, katika sehemu zote hizoTanzania imekuwa nchi bora zaidi kwani pamoja na mazingira bora ya kazi zetu lakini pia wakandarasi wazawa wamekuwa wakipewa nafasi katika miradi ya ujenzi,” alisema Hu Bo.
Kwa mujibu wa Hu Bo tangu mwaka 1977 kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi nchini Tanzania, hatua inatokana na ushirikiano na uhusiano wa kirafiki uliopo baina ya Serikali ya China na Tanzania.
Alitaja baadhi ya miradi ya Serikali iliyokamilishwa kampuni hiyo nchini ni pamoja na ujenzi wa ukumbi wa Bunge Dodoma, Jengo la Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Jengo la Ofisi ya Wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar, Ofisi za Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).