Wachimbaji wadogo 15 waliokuwa wamefukiwa na kifusi kwenye Mgodi wa RZ, Nyarugusu mkoani hapa jana waliruhusiwa kutoka hospitalini baada ya hali zao kuendelea vizuri. Juzi Jumapili, ilikuwa siku ya muujiza kwa watu hao ambao waliishi chini ya ardhi kwa zaidi ya saa sabini na mbili (72) kabla ya baadaye kuokolewa katika tukio hilo la kihistoria nchini Tanzania.
Januari 25, 2017, watu hao, akiwemo raia mmoja wa China, Meng Juping walifukiwa na kifusi kwenye mgodi huo na hivyo kuishi ardhini kwa muda huo bila kuona jua wala mwanga, hali ambayo kimaumbile ni vigumu kutokana na kukosa hewa safi ya oksijeni ambayo ndiyo humfanya binadamu kuishi.
Kufuatia muujiza huo ambao wengi wanaamini ni Mungu tu kwa binadamu kuishi chini ya ardhi, Uwazi lilizungumza na daktari wa magonjwa ya binadamu jijini Dar, Godfrey Chale ambaye alitoa sababu zilizowasaidia wahanga hao kukiepuka kifo licha ya kuishi ardhini.
“Kikubwa ni kwamba, inategemea watu walipo. Mfano, kama hao jamaa wote kumi na tano walikuwa eneo lenye nafasi au ‘hall’ kubwa kule ardhini, hiyo ndiyo ilikuwa salama yao.
“Unajua binadamu tunaishi kwa kutegemea hewa ya oksijeni, sasa inapotumiwa na watu halafu haingii nyingine, ni lazima watu wafe. Lakini kama watu watakuwa kwenye eneo lenye uwazi mkubwa kama nilivyosema wanaweza kudumu kwa siku kadhaa kwa sababu oksijeni bado ipo.
“Lakini kama walikuwa kumi na tano halafu kwenye nafasi ndogo ni vigumu sana kuendelea kuishi. Kwa sababu ushindani wa kuvuta oksijeni ungekuwa mkubwa, wangekufa.
“Hili sasa linategemea na idadi ya watu kwani pia inawezekana wale walikuwa kumi na tano kwenye nafasi kubwa, wangekuwa zaidi ya idadi hiyo, mfano thelathini na ukubwa wa eneo ni huohuo, lazima wangepoteza maisha kwani oksijeni ingekwisha haraka.
“Kingine kilichowaokoa ni siku za kukaa na kuokolewa, kwani pia kama wangekaa muda zaidi ya siku hizo, lolote lingeweza kutokea kwani oksijeni pia ingeisha. Ndiyo maana utaona watu kama wale wakishatolewa lazima waongezewe maji ili waweze kurejea katika hali ya kawaida kwani miili yao inakuwa imepoteza nguvu kwa kiu, njaa na kuvuta hewa kwa tabu,” alisema Dokta Chale.
Kuhusu madhara yatokanayo na kuishi ardhini kwa siku hizo, Dokta Chale alisema kuwa, ni kusumbuliwa kwa mfumo wa kuvutia hewa.
“Unajua mtu akiwa chini ya ardhi lazima atakuwa anavuta hewa yenye vumbi na uchafu mwingine. Kwa hiyo lazima tiba yao itakuwa pamoja na kuangalia mfumo wa kuvutia hewa,” alisema daktari huyo anayetoa huduma kwenye Hospitali ya Wilaya ya Temeke, Dar.
Waliofukiwa katika mgodi huo ni Ezekiel Bujiku (20), mkazi wa Wigo, Yohana Shigangama (34) na Busanda John (20) (mahali wanakoishi hakujajulikana), Aniset Masanja (32), mkazi wa Katoro na Dikson Moris (25) ambaye naye haikujulikana alikokuwa akiishi. Wengine ni Mussa Cosmas (28), mkazi wa Tabora, Raphael Nzubi (26), mkazi wa Bariadi, Amani Sylvester (26), mkazi wa Sengerema, Sheku Butogwa (22), mkazi wa Nyamalulu, Hassan Idd (31) mkazi wa Ilemela,
Augustino Robert (27), mkazi wa Nyarugusu, Mgalula Kayanda (23), mkazi wa Ramadi, Sabato Philimon (30), mkazi wa Musoma, Meng Juping (36), raia wa China na mwingine ambaye jina lake halikutambulika mara moja.
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, ameagiza kurudishwa kwa Afisa Madini wa Mkoa wa Geita, Fabian Mshai ambaye alihamishwa, ili kutoa maelezo juu ya uzembe uliosababisha tukio hilo.