MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif
Sharif Hamad watafunga mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge
wa Jimbo la Dimani unaotazamiwa kufanyika jumapili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Ofisi Makao Makuu ya CCM
Kisiwandui jana Dk Shein atafunga mikutano ya kampeni za kumnadi mgombea
wa CCM Juma Ali Juma ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.
Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar, Idara ya
Itikadi na Uenezi Waride Bakari Jabu alisema kampeni hizo zitafikia
tamani kwa Dk Shein kuhutubia mkutano wa mwisho wa kampeni.
“Kampeni zitafikia tamati kwa kupata baraka kubwa za Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Dk Shein,” alisema.
Juzi akizungumza katika mkutano wa kampeni Bweleo, mgombea wa CCM
Juma alisema atahakikisha vikundi vya wajasiriamali wanawake vinapewa
kipaumbele kwa kupatiwa mitaji ya kuendesha biashara zao.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif anatazamiwa
kufunga mkutano wa kampeni za uchaguzi mjini Fumba Mkoa wa Mjini
Magharibi Unguja.
Chama cha CUF katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani kimemsimamisha
mgombea wake Abdulrazak Khatib. Jumla ya vyama vya siasa 12 vinashiriki
katika uchaguzi huo huku chama cha CCM na CUF vikionesha kuwepo mchuno
mkali.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo
hilo Hafidh Ali Tahir (CCM) aliyefariki akiwa katika mkutano wa Bunge
mjini Dodoma mwaka jana.
Mapema jana Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilisisitiza kwamba
watu watakaopiga kura ni wale ambao wamesajiliwa katika daftari la
kudumu la wapiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka. 2015.
Mkurugenzi wa ZEC Kassim Ali alisema ni matarajio yao kuwa wapiga
kura na wananchi wa Jimbo la Dimani watashiriki katika uchaguzi mdogo
kwa njia ya amani na kuheshimu demokrasia.