AWALI ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutulinda, kutupa uhai na afya njema hadi leo. Yote yamewezekana kwa kuwa amependa sisi wajoli wake tuwe hai na wenye afya.
Wako wenzetu wakati huu wako hospitali au vitandani kutokana na maradhi mbalimbali. Tuwaombee wote walio wagonjwa.
Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujua kwanini wengine kawapa afya njema na wengine kawapa maradhi ya aina mbalimbali. Inawezekana kati ya mnaosoma makala hii sasa, wengine hamtaweza kuuona mwaka 2018.
Ndugu zangu Watanzania, ili tuweze kuwa na matumaini ya mwaka mpya wa 2017 tuliouanza, ni vema takatafakari mwaka tunaouaga wa 2016.
Huu ni mwaka wa kwanza tangu Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, ambapo tulimpata Rais mpya, John Magufuli na kuunda serikali yake. Ni dhahiri kila tunapoingia kwenye uchaguzi, kila mmoja wetu huwa na matumaini ya matokeo ya uchaguzi kuleta unafuu katika maisha yetu ya kila siku.
Ndio maana wakati wa kampeni, tunasikiliza kwa umakini sera mbalimbali zinazoletwa kwetu. Hatimaye tunapiga kura kuichagua ile sera ambayo kila mmoja kwenye nafsi yake anaamini itamletea unafuu, itamtoa pale alipo kuelekea kwenye maisha bora.
Kwa wengine ni matumaini ya kutoka kwenye maumivu ya maisha kwenda kwenye unafuu. Kwa uzoefu wangu wa ubunge wa miaka 15 na miaka 20 kwenye siasa( active politics), ninaelewa kabisa kuwa wako ambao siku ya pili baada ya uchaguzi wanataka kuona kero zao zimeondoka.
Kama tatizo lilikuwa maji safi na salama, hawaelewi, baada ya kumpata kiongozi kwanini siku ya pili, ya tatu, mwezi na hata mwaka baadaye hakuna maji!
Hii ni hali ya kawaida kwa binadamu. Mimi nilichaguliwa na watu wa Karatu kutokana na kero kubwa ya maji wilayani Karatu. Maji yalidhalilisha utu wa binadamu hasa akinamama.
Maji yalifanya watoto wadogo kubakwa kwenye vituo vichache vya maji vilivyokuwepo. Maji yalifanya mahudhurio ya watoto shule za msingi yadorore kwa kuwa watoto walikesha usiku kucha kusubiri maji kwenye vituo vichache vya maji.
Nakumbuka kila nikipita mitaani, nilianza kuitwa tapeli kwa kuwa miezi sita baadaye, na kisha mwaka mmoja baadaye, maji yalikuwa hayajaonekana kwao. Mwananchi wa kawaida yeye hajui jitihada unazofanya kuleta maji.
Yeye kazi yake ilikuwa kupiga kura, mengine hayamhusu. Hajui kuwa maadui zako wanakuhujumu na kukuvuta chini ili usifanikiwe, kwani kufanikiwa kwako ni kuonyesha udhaifu wao.
Mwananchi haelewi kuwa mikakati ya utekelezaji wa mradi wowote haina budi kuandaliwa kwa umakini, fedha zitafutwe, kazi ya usanifu lazima ifanyike.
Kwa Karatu, maji yalianza kutoka kwenye mabomba mwaka 2000, wakati uchaguzi ulikuwa 1995. Tone la kwanza la maji lilipotoka, wananchi hata waliokata tamaa, waliodhani wametapeliwa walilipuka kwa furaha ya ajabu.
Walisahau matusi yote waliyokuwa wamenishushia. Sasa wakaanza kubaini kwamba kumbe hawakuwa wakidanganywa. Waliokuwa wavumilivu waliona na kushuhudia hatua zote za utekelezaji wa mradi.
Waliokuwa wepesi kukata tamaa nusura watukatishe tamaa sisi watekelezaji kwa kejeli, kebehi, matusi tuliyokuwa tukimwagiwa mitaani.
Uvumilivu ulizaa matunda. Wananchi takribani 30,000 walipata maji ya uhakika ndani ya nyumba zao, wengine katikati ya kitongoji chao, vitongoji vingine vilikuwa na DP ( Distribution Points) zaidi ya mbili au tatu.
Hivyo mama anaenda na sufuria na akirudi anabandika jikoni. Hili ni tunda la uvumilivu. Ndugu zangu nimeeleza kidogo kwa kirefu hadithi hii ambayo ilinipata mimi na wananchi wangu wa Karatu.
Ninafahamu pia kwamba mara baada ya ushindi wa Magufuli, makundi tofauti ya wananchi yatakuwa na matumaini tofauti kuhusu matarajio ya nini watakachokipata.
Wamachinga walijua mikopo midogo midogo itapatikana kwa urahisi, na hawatakimbizwa tena mitaani kama mbwa. Bodaboda waliozuiliwa kuingia katikati ya miji walijua sasa wamefunguliwa milango na hivyo biashara yao itakuwa rahisi.
Hali hii iko hivyo kwa takribani makundi yote ya kijamii. Kwa miaka mingi, wananchi wetu wameaminishwa kuwa nchi yetu ni tajiri na hivyo wana matarajio makubwa kwa viongozi wao.
Tuna rasilimali za kila aina kuanzia rasilimali chini ya bahari na maziwa yetu, magogo kwenye misitu yetu, rasilimali wanyamapori, ikiwa ni pamoja na “twiga wetu” aliyekunjwa shingo na kuingizwa kwenye ndege kutoroshwa.
Kuna kero nyingine pia kama vile maelfu ya tembo na faru waliokuwa wakiuawa bila huruma na majangili kwa manufaa yao binafsi, fedha zetu kwenye benki kuibiwa hovyo nakadhalika.
Wananchi haohao wamesahau kuwa mara baada ya uchaguzi, kazi kubwa ni mapambano dhidi ya “ wahujumu hao”. Kwa bahati mbaya “mpira usiocheza hujui si rahisi kujua ugumu wake. Kumbe hata ukiachiwa peke yako ufunge bao kwenye goli lililo wazi, unaweza kuupaisha juu kwa mshangao wa wengi!”
Hivi ndivyo ilivyo kwa serikali. Natambua kabisa watumishi wa umma walitegemea mishahara itapanda na kukidhi mahitaji yao, wanafunzi wa vyuo walijua mikopo sasa itakuwa rahisi na itatoka kwa wakati.
Wazazi walijua “ elimu itakuwa bure hadi kidato cha nne” na hawatasumbuliwa tena, hata kero ya madawati itatatuliwa bila mwananchi kuguswa kabisa! Natambua kuwa matamanio hayo si tu hayakutekelezwa bali maumivu yalikuwa makubwa zaidi kwa mwaka wote wa 2016.
Mitaji imepotea, mabenki hayakukopesha kwa hofu mbalimbali, mzunguko wa fedha ulikauka, hata wenye mitaji yao midogo ikaliwa. Hoteli nyingi kufungwa kwa kushindwa kulipa mikopo kutokana na kutokupata wateja.
Watumishi wa umma hawakupewa mishahara iliyotangazwa kupanda. Hii ni hali ngumu na ninatoa pole sana kwa wale wote, kwa makundi yao, walioumia kwa namna moja au nyingine.
Kazi ya kwanza ya kiongozi yeyote makini anaposhika dola ni kuangalia mianya mbalimbali ya wizi na uozo wowote katika usimamizi wa rasilimali za umma. Nadhani wote tunakiri serikali hii ilipoingia tu madarakani, jambo la kwanza lilikuwa kubaini wafanyakazi hewa.
Leo tunazungumzia wafanyakazi hewa takribani 20,000. Fikiria ni mabilioni mangapi kwa mwezi yalienda kwa wafanyakazi hewa? Ni dhahiri fedha hizi zingelitengeneza mzunguko wa fedha kama zingelikuwa kwenye mkondo sahihi. Hakuna shaka kwenye hilo.
Lakini ni wafanyikazi hewa, hivyo taifa halikuzalisha kutokana na wafanyakazi hao hewa. Ghafla uhakiki unaonyesha kuwa kuna siyo tu waalimu hewa, lakini wanafunzi hewa zaidi ya 60,000. Mungu atusamehe!
Sijui tumelogwa! Taifa la ajabu. Watu “wanatumbua” bila aibu. Hawa walikuwa wakitumbua fedha zetu kwa manufaa ya “ matumbo yao” na familia zao.
Hatujakaa sawa tukaambiwa kuwa hata fedha za TASAF zilizolenga kusaidia kaya maskini sana nazo zimeliwa. Kaya takribani 55,000 zilizokuwa zinufaike zimekosa huku baadhi ya viongozi wa serikali wa ngazi mbalimbali, wakiwemo maofisa wa TASAF wenyewe wakidaiwa kuhusika na wizi huo.
Hatujatulia mara maelfu ya wanafunzi ambao hawakuwa na sifa za kujiunga na elimu ya Chuo Kikuu walipewa nafasi! Ni dhahiri kuwa wazazi wa watoto waliofukuzwa wameumizwa na hatua hii.
Lakini ipi nafuu kuendelea kuwa nao na kuathiri ubora wa elimu hasa katika dunia ya leo ya ushindani. Wenzetu kila siku wanapambana na ugunduzi wa mipango ya kwenda kwenye sayari mbalimbali kwa lengo la kutafuta sayari yenye kufaa kwa maisha ya binadamu.
Sisi tutaendelea kuwa na mijadala ya kutafuta fefha kwa matundu ya choo. Hadi lini! Najua lilikuwa uamuzi Mgumu sana Mhe. Rais na Waziri wako wa Elimu. Lakini hapakuwa na njia.
Nashukuru kama wazazi mlifanya jitihada za kuwaelekezea vijana hao penginepo ili rasilimali watu za Taifa zisipotee na wao pia wanufaike na rasilimali za Taifa lao. Ni haki yao.
Haikuishia tu kwenye fedha. Bandarini Kontainer zaidi ya 11,000 zinaingizwa bila kulipiwa kodi na ushuru mbalimbali. Hii ikasababisha milango na mirija ya ukwepaji kodi kufungwa.
Na dhihiri waliokuwa wakinufaika na kupata “ super profit” kwa kukwepa kodi wataikimbia Bandari yetu. Kitendo cha kuikimbia Bandari, kwa muda athari yake ni kuwa bidhaa zitapungua, na makusanyo ya kodi za Serikali pia yatapotea.
Mzunguko wa fedha katika ujumla wako nao utapungua. Na hivyo hali ya maisha kuwa ngumu kwa kila kundi.
Ndugu zangu, kwa kiongozi yeyote jasiri, mwadilifu, mpenda Taifa lake anakutana na mtihani mkubwa sana. Aidha ni uchaguzi mgumu. Au aache uozo huo wote kuanzia “ hewa” hadi “ ukwepaji kodi uendelee au audhibiti kwa njia zote zinazowezekana.
Akiuruhusu maana yake nimkuwa mzunguko bandia wa fedha utaendelea kuwepo na kundi dogo linalofikiwa na mzunguko huo litaendelea kunufaika lakini umma mpana utaendelea kuumia, kama tulivyokuwa tukiumia kabla ya uchaguzi.
Kwa bahati mbaya walio wengi ambao walikuwa hawanufaiki na uozo uliokuwa ukiendelea hawakuwa na pa kusemea. Leo angalau wamempata Rais anayewasemea wao. Rais amekuwa akitumia neno “wapiga dili”.
Ni kweli waliokuwa wakinufaika ni hao wapiga dili waliotengeneza “ wafanyikazi hewa, hewa, hewa, kila sekta”.
Lakini kwa bahati mbaya wanaoathirika ni pamoja na mama lishe, na wafanyibiashara ndogo ndogo ambao kimsingi hawahusiki kwa lolote lile na kupiga dili.
Wao wanafanya biashara wakati hao wachache wakipiga dili. Lakini hapa ndipo palipo na msemo, “mtego wa panya kuwakamata wahusika na wasiohusika”. Hii ndio inayoitwa “Dilemma”.
Unachagua kipi? Uache uozo na ufisadi/ huu mkubwa uliofilisi nchi nzima uendelee kwa ajili ya kuwasaidia wenye biashara ndogondogo au funga njia, kwa muda tutaumia, rudisha nchi kwenye reli na baada ya muda fungua milango kwa biashara halali.
Kweli kwa uamuzi huu liko kundi litaumia sana. Lakini taifa likirudi kwenye reli, kundi hilo na wote tutanufaika. Taifa zima litanufaika.
Nina hakika tukiisha kurudi kwenye mstari ajira zitatoka kwa utaratibu unaotakiwa, fedha za miradi zitatoka na mzunguko wa fedha utarudi kama kawaida. Maamuzi magumu yanahitaji kushirikiana lakini pia uvumilivu mkubwa. Hakuna jambo jema linapatikana kirahisi.
Najua kuwa kuna wengi wanalalamika. Wako wasomi kati yao. Lakini kama wasomi hao wana dhamira njema, miaka yote nchi ilipokuwa inatopea kwenye dimbwi la ufisadi, uwizi huu; mbona walikaa kimya?
Mbona hatujusikia sauti yao. Wasomi hao wengine wao si ndio walikuwa pia wakikusanya mamilioni wakati mwingine kwa “Dola Za Marekani” kwa kilichokuwa kikiitwa kazi za kiushauri yaani Consultancies?
Wengine walikuwa wakiandika rasimu za sheria mbovu lakini wakiishia kujikusanyia mamilioni ya fedha. Kwa bahati nzuri sizungumzii nadharia. Ninayafahamu yote ninayosema kwa undani.
Mambo ya “ Watumishi hewa”, wanafunzi hewa Kamati ya Bunge ya Hesabu ya Serikali za Mitaa tulianza kuyazungumzia mwaka 2007. Mbona tangu wakati huo wakati huo hatukumwona msomi yeyote akifanyia utafiti ( hata baada ya kuwarahisishia kwa taarifa za LAAC).
Tuache kudanganyana. Hawa wasomi wetu hawakuona huo ufisadi , wizi na uozo huu wakati ulipoanza ? Leo ndiyo wanaona uchungu au kwa sababu kwa namna moja au nyingine na wao pia wameguswa? Japo si wasomi wote.
Watu wanalalamikia safari za nje kuzuiwa. Tena wanaihusisha na mgawanyo wa mamlaka na kuwa Rais anaingilia mamlaka zingine. Hivi mwaka 2014 nilipotaka Bunge kufanyiwa “Special Audit” kwa ziara za kibunge zilizokuwa zikitumbua fedha bila manufaa kwa taifa walikuwa wapi?
Ni sekta ipi katika nchi yetu ambayo haikuguswa na Ufisadi? Hatimaye mwajibikaji mkuu wa fedha za Umma ni Rais kwa mujibu wa Katiba. Iweje basi akichukua hatua ionekane kuwa ameingilia mamlaka zao?
Ni kweli siyo kila kitu cha Serikali ya Awamu ya Tano mimi naunga mkono. Mimi siungi mkono kujenga reli kwa fedha nyingi kwa Standard Gauge. Labda tuambiwe kuwa wakati inajengwa kwa Standard Gauge wanazungumzia pia Electrification.
Nilikwishasema “ we do not have to re- invent the wheel”. Leo unatoka Hamburg kwenda Munich Ujerumani takribani umbali wa kilomita 1500 kwa muda wa saa 3 tu. Sisi tunakwenda Dar- Mwanza na treni inachukua siku tatu hadi nne.
Hii ni karne ya sayansi, hatuhitaji kuwekeza fedha kama hatutaenda kisasa. Inatakiwa mtu alalale nyumbani kwake Mwanza anaenda kufanya kazi Dar na kinyume chake.
Tunataka bidhaa za viwanda na za kilimo zizalishwe kwa wingi Mwanza, Mbeya na Kigoma na zifike katika Bandari ya Dar es Salaam kwa muda usiozidi saa tatu na si baada ya wiki.
Nchi hii haiwezi kuendelea kwa namna ya kufikiri ya mwaka 1947. Wasomi wetu wana jukumu la kujitafakari na kubadilisha namna yao ya kufikiri na kutoa mchango kwa taifa kama wanahitaji tuwatambue kwa usomi wao.
Wanasiasa wetu nao ajenda isiwe kuingia Ikulu pekee. Ajenda iwe namna ya kuliondoa taifa kwenye “ mduara” ( Vicious Circle) tulioko na mkakati walio nao wa kulipeleka taifa tunakotaka.
Kwa ujumla nchi ilikosa mtu wa kusimamia rasilimali. Nchi ilikosa mtu wa kutoa maagizo na maamuzi. Nchi ilikosa usimamizi na mtu wa kukemea. Rais JPM amejidhihirisha kuwa anayo nia, anayo dhamira na anao ujasiri na uwezo wa kufanya.
Chanzo: Gazeti la Raia Mwema, JAN 05, 2017.
Mwandishi wa makala hii aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Jimbo la Karatu kupitia chama hicho.
Tawile baba........kwa sasa mafisadi 'wanakodo-kodo' ...HAPA KAZI TU!
ReplyDelete