Nahodha
wa Yanga, Haruna Niyonzima, amesema kuwa anaamini kocha wao George
Lwandamina atakipeleka mbali zaidi kikosi hicho kwenye michuano ya
kimataifa na kutwaa ubingwa wa ligi kutokana na ubora wake na kudai kuwa
kinachotakiwa apewe muda na si watu kuanza kumlalamikia kwa matokeo
yoyote yatakayopatikana.
Kumekuwa
na tuhuma kuwa Lwandamina amekuwa akiwapa mazoezi magumu wachezaji wake
hadi siku ya mechi, hivyo kusababisha wachezaji hao kuchoka na
kushindwa kufanya vyema kwenye mechi.
Niyonzima
amesema kuwa, siyo wakati muafaka kwa sasa kutoa lawama kwa kocha huyo
kwa kuwa bado hajakaa na timu kwa muda mrefu, hivyo anahitaji kuyasoma
mazingira kisha ndipo aweze kufanya vyema.
“Lwandamina
ni mwalimu mzuri na tunamuelewa sana tofauti na watu wanavyodhania, pia
watu wanahitaji kutambua kuwa, kocha huyo anatakiwa apewe muda wa
kutosha kuweza kuinoa timu hiyo na hasa ukizingatia yeye ni mgeni, hivyo
hawezi kukopi kila kitu kwa wakati mmoja.
“Anatakiwa
kupewa muda wa kuweza kuelewa kila kitu ndipo aweze kufanya kazi yake
ipasavyo na si tuhuma ambazo amekuwa akipewa kwani naamini atatufikisha
mbali zaidi kwenye ligi na mashindano ya kimataifa,” alisema Niyonzima.
Aidha,
alimalizia kwa kusema kuwa, anaamini wataweza kufanikiwa kutetea
ubingwa wa ligi kwa kuwa wamejiandaa vyema, licha ya kutambua kuwa
mzunguko wa pili ni mgumu na wanahitaji kujipanga na kujituma ili waweze
kufanikiwa kutetea taji lao hilo.