MSHITAKIWA Emmanuel Mkenya aliyefikishwa kwenye Mahakama ya Mwanzo Kariakoo jana kusomewa mashitaka ya uzembe na uzururaji, ametoroka mikononi mwa polisi baada ya kujipaka kinyesi mwilini.
Mshitakiwa huyo alifikishwa asubuhi mahakamni hapo kujibu mashitaka yanayomkabili na kuwekwa mahabusu kusubiri kuitwa.
Muda wa kusomewa kesi ulipofika, askari alikwenda kumwita yeye na wenzake ili wapande kizimbani, lakini mshitakiwa huyo alitoka akiwa amejipaka kinyesi chake, alichojisaidia kwenye choo cha ndani ya mahabusu.
Huku akionekana kujiamini, mshitakiwa huyo badala ya kupanda kizimbani, aliondoka taratibu kupitia lango la kutoka nje ya Mahakama, huku polisi wakishindwa kumkamata kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Baada ya kutoka nje, mshitakiwa mwenzake kwenye kesi hiyo ya uzembe na uzururaji, alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Agnes Barasobian.
Hata hivyo, kabla ya Karani Hatanawe Kitogo kusoma mashitaka dhidi ya mshitakiwa wa pili, Hakimu Agnes aliuliza alikokuwa mshitakiwa namba moja.
Polisi aliyekuwa mahakamani hapo alimjibu Hakimu kuwa mshitakiwa huyo alitoroka baada ya kujipaka kinyesi mwili mzima.
Hakimu Agnes akionesha kukasirika, alimtaka askari huyo ahahakishe mshitakiwa anatafutwa na kukamatwa, kwani haiwezekani aondoke mahakamani huku akiwa na mashitaka yanayomkabili.
Alisema hakubaliani na sababu za askari huyo, kwa kuwa anatambua kuwa kwenye mafunzo ya kijeshi, hupewa mbinu za kukabiliana na washitakiwa.
Washitakiwa hao walikamatwa na Koplo Luseseko Januari 19 Msimbazi, Dar es Salaam wakituhumiwa kwa uzururaji. Kesi hiyo iliahirishwa jana hadi Januari 30 itakapotajwa.