KOCHA Msaidizi wa timu ya soka ya Simba, Jackson Mayanja amesema
baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana na Mtibwa Sugar katika mechi ya
Ligi Kuu juzi, nguvu zote sasa zinaelekezwa kuikabili Azam kwenye
mchezo wao wa Januari 28.
Mayanja, alisema hayo juzi baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya
Mtibwa Sugar uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini hapa, ambapo
matokeo hayo ya sare ya bila kufungana yameifanya Simba iongoze ligi kwa
tofauti ya pointi mbili kutoka nne za awali.
“Mchezo haukuwa mbaya, wachezaji wamecheza vizuri, lakini hawakuweza
kupata magoli licha ya kupata nafasi zaidi ya mbili za kuwezesha kupata
ushindi,” alisema Mayanja.
“Tumemaliza mchezo wetu na Mtibwa Sugar na kuambulia pointi moja, na
sasa tunaelekeza nguvu kwenye mchezo wetu na Azam… huko tunajiandaa na
ushindi,” alisema Mayanja.
Mayanja alisema baada ya mchezo huo wanajipanga kufanya mazoezi kwa
ajili ya kukabiliana na Azam, na kutabiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu
kulingana na historia ilivyo kwa timu hizo kwa siku za hivi karibuni
zinapokutana.
“Siwezi kuizungumzia sana Azam kwavile mechi hiyo bado lakini tunajipanga vizuri kuikabili kwenye mchezo huo,” alisema Mayanja.
Simba ilikutana na Azam kwenye fainali za Kombe la Mapinduzi Zanzibar
hivi karibuni na kulala kwa bao 1-0, matokeo yanayotabiri ugumu wa
mechi ya marudiano ya timu hizo. Katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa
Ligi Kuu Simba ilishinda.
Aidha, Mayanja alisema kupata ushindi ugenini ni jambo gumu na
linachangiwa na sababu mbalimbali hivyo wanajiandaa kukabili michezo za
ugenini katika michezo ijayo. Pamoja na hayo, aliisifu Mtibwa Sugar kwa
kucheza vyema katika mchezo huo tofauti na iliyokuwa mchezo wao wa
kwanza uliofanyika Jijini Dar es Salaam.