WIKI zilizopita, aliyekuwa mmoja wa wapiganiaji utawala wa wengi
Afrika Kusini, Askofu Desmond Tutu, wa Kanisa la Anglikana,
akiadhimisha mwaka wa 85 wa kuzaliwa kwake, alisema anategemea kutoa
maombi ya kufanyiwa ‘mauaji ya huruma’ kwa madaktari iwapo hali yake
ikitokea kuzorota kadri umri unavyozidi kusonga mbele.
“Ninataka kuyamaliza maisha yangu kwa kifo cha kusaidiwa. Watu
wanaokabiliwa na kifo wana haki ya kuchagua jinsi ya kumwacha Mama Dunia
kwa heshima,” aliandika katika gazeti moja akiisifia Canada na Jimbo la
California (Marekani) ambako wagonjwa wanaokabiliwa na magonjwa yenye
maumivu na mateso makali huruhusiwa kifo cha heshima.
‘Mauaji ya huruma’ aliyokuwa akiyamaanisha Tutu ni yale yatolewayo
kwa watu wanaougua magonjwa yenye maumivu na mateso makali na ambayo
mwisho wake ni kifo. Mauaji hayo kwa Kiingereza huitwa ‘Euthanasia’
(hutamkwa Yuthenazia). Euthanasia ni neno lenye asili ya Kigiriki
ambalo humaanisha ‘Kifo Kizuri”.
Vifo vya Euthanasia viko makundi makuu matatu: Euthanasia ya Hiari
(yenye kibali cha mgonjwa na ndugu zake), Euthanasia Isiyo ya Hiari
(inayofanyika kwa kukosekana kibali cha mgonjwa, hususan mtoto mdogo
asiyeweza kusema au kujieleza) na Euthanasia ya Lazima (inayofanyika
bila kibali cha mgonjwa au dhidi ya utashi wake).
Euthanasia ya Lazima — ni haramu duniani kote na huchukuliwa kama
mauaji ya kukusudia. Njia kuu za ‘mauaji’ hayo ni pamoja na kutompa
tiba mgonjwa au kumdunga sindano ya sumu. Hata hivyo, kuna migongano
kuhusu Euthanasia duniani ambako wapinzani hutetea maisha ya mtu
lazima yaheshimiwe hadi mwisho, wakati wanaounga mkono husema ni lazima
mtu anayeteseka kwa ugonjwa aruhusiwe kufa kwa heshima.
Miongoni mwa nchi ambako Euthanasia ni halali ni pamoja na Netherlands (Uholanzi), Colombia, Belgium, na Luxembourg.
Nchini Marekani, Euthanasia ni haramu, lakini kuna njia wanazoruhusiwa
madaktari, katika majimbo kadhaa, kuzitumia katika kumsaidia mgonjwa
‘kujiua’.