NYUMBA 49 zimeezuliwa na kubomolewa huku Neema Masunga (27)
akipoteza maisha kwa kupigwa na radi kutokana na mvua iliyoambatana na upepo na
radi kunyesha kwenye machimbo ya Matabe kijijini Bwanga wilayani Chato mkoani Geita.
Katika tukio hilo, la juzi nyumba 11 zilibomolewa na 38
kuezuliwa mapaa na kusababisha familia kukosa mahali pa kuishi na wengine
kulazimika kujihifadhi kwa majirani.
Tukio hilo lilitokea saa mbili usiku baada ya mvua iliyoambatana
na upepo mkali na ngurumo za radi kunyesha kwa nusu saa.
Mwenyekiti wa eneo hilo, Jackson Kusekwa alisema marehemu
Neema ameacha watoto watano, mmoja akiwa wa wiki mbili.
Alisikitishwa na tukio hilo lililotokea kwenye kipindi
kigumu cha njaa kwa waakzi wa Matabe baada ya mazao waliyolima yakiwamo mahindi
kukauka kwa jua.
Alisema Neema alipoteza maisha baada ya kupigwa na radi
akiwa chumbani akimnyonyesha mwanawe huyo ambapo radi ilimrusha hadi
sebuleni na kufariki dunia.
“Radi ilimrusha hadi sebuleni na mtoto akabaki
chumbani…imeharibu sana nyumba kwani imepasuka, kwa ujumla tuna hali mbaya sana,
wananchi kwa sasa wanaishi kwa shida wengine wamehamia kwa majirani ili
kujihifadhi baada ya nyumba zao kubomolewa,” alisema Kusekwa.
Mmoja wa wanakijiji, Abel Charles alisema baada ya hali
hiyo wananchi walikusanya mabati yaliyoezuliwa na katika harakati hizo walipata
taarifa za mtu kufariki dunia na ndipo wananchi walijikusanya na kwenda eneo la
tukio na kushuhudia mwanamke huyo akiwa amepoteza maisha.
Mama mzazi wa marehemu, Mariam Masunga (78) alisema,
binti yake amemwachia watoto hao na mdogo kabisa anayehitaji msaada kwani hata
yeye kwa umri wake alikuwa akimtegemea mwanawe huyo.
“Naomba msaada wa kulea watoto hawa...mimi sina uwezo,
kwani nimezeeka katika maisha yangu nilikuwa namtegemea mwanangu ambaye sasa
amefariki dunia, naiomba Serikali inisaidie,” alisema Mariam huku akiangua
kilio.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya
ya Chato ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Shabaan Ntarambe alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kudai kuwa alituma wajumbe wa kamati yake kufuatilia kabla ya
kutoa taarifa hizo.
“Nimemtuma OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) kufuatilia hilo
tukio; ni kweli limetokea akishatoka huko nitatoa taarifa baadaye,” alisema
Mkuu wa Wilaya.
NB:Wilaya ya Chato Iko Mkoa wa Geita anapotoka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli.