Mwenyekiti wa CUF
anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim
Lipumba na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Frederick Sumaye wamekutana
kwenye kampeni za uchaguzi wa diwani wa Kata ya Kahumulo huku kila mmoja
akirusha vijembe kwa chama cha mwenzake.
Wakati
Lipumba akiielezea Chadema kuwa imepoteza mwelekeo kwa kumkaribisha
waziri huyo mkuu wa zamani na mwenzake, Edward Lowassa, Sumaye amesema
CUF haiwezi kuwakomboa wakazi wa Kahumulo.
Wawili
hao walikuwa katika kata moja wakiwanadi wagombea udiwani wa vyama vyao
katika mikutano miwili tofauti ya uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika
Jumapili ijayo.
Akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara wa kumnadi Ntalikwa Ishatala uliofanyika Kata
ya Kahumulo, Profesa Lipumba amesema Chadema ni chama kilichopoteza
mwelekeo kwa kuwa kimebeba mafisadi waliohama CCM.
Wakati
Profesa Lipumba akiishambulia Chadema, Sumaye alikuwa eneo jingine
akimnadi mgombea wa chama hicho kwenye kata hiyo, Dotto John.
Waziri huyo mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu amesema CUF na CCM ni vyama ambavyo havina mtazamo wa kuikomboa Tanzania.